ROSE MUHANDO KUPAMBA TAMASHA LA SHANGWE MKOANI KAGERA, DESEMBA 9


MWIMBAJI maarufu wa muziki  wa Injili nchini, Rose Muhando na mwenzake Enock Jonas (Zunguka) wanatarajiwa kutia chachandu katika tamasha la kwanza kubwa kufanyika Mkoani Kagera.
 
Tamasha hilo la Shangwe Kagera lina lengo la kuielimisha jamii na kuamsha mwamko wa kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika maisha magumu.
 
Mkurugenzi wa Kampuni ya Beula Communications Ltd, ambao ni waandaji wa tamasha hilo,Melkizedeck Mutta anasema kuwa matayarisho ya tamasha hilo yanaendelea vizuri kutokana na mwitikio mkubwa wa watu mbalimbali waliojitokeza kushiriki.
 
Pia, Mutta anasema bendi ya muziki ya wazawa mkoa huo, Kakau Band pamoja na vikundi vingine vya wanakwaya  wa makanisa mbalimbali, kikundi cha watoto yatima wanatarajia pia kutumbuiza.
 
Mutta anasema tamasha hilo la aina yake  linatajiwa kufanyika  Uwanja wa Kaitaba na pia kwenye ukumbi wa Lina’s mjini Bukoba, siku ya Uhuru, Desemba 9.
 
“Mpaka sasa tumekamilisha sehemu kubwa ya matayarisho hayo ikiwamo kulipia  uwanja pamoja sehemu ya malipo kwa wasanii ambao watashiriki,” alisema.
 
Pia, mkurugenzi huyo aliwaomba wadhamini zaidi na wadau wengine wa maendeleo na watoto kujitokeza kushiriki ili kuwasaidia jamii hasa watoto yatima na wengine wanaoishi katika mazingira magumu.
 
 

Comments