SIMBA YATOA TAHADHARI KWA MWAMUZI WA MCHEZO WA KESHO


Ezekiel Kamwaga, ofisa habari wa Simba
WAKATI mechi  ya mahasimu wa soka nchini Simba na Yanga ikirindima kesho , klabu Simba imetoa angalizo kwa mwamuzi wa mchezo huo Mathew Akrama wa Mwanza kufuata sheria 17 za mchezo. 
Timu hizo zitakutana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kuanzia saa moja kamili usiku. 
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema wameshangazwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),kumpanga Akrama kuchezesha mechi mbili mfululizo za Yanga katika hiyo. 
Alisema katika mchezo huo wa Jumapili ambao Yanga ilicheza na African Lyon, awali Tff ilikuwa imepangwa mwamuzi Amon Paul wa Mara, kabla ya kumbadilisha na kumuweka Akrama. 
“Kwa hali kama hiyo lazima tupate na wasiwasi kidogo, ila yote kwa yote tunamuomba mwamuzi afuate sheria 17 za mchezo kwani mechi hiyo  inagharimu maisha ya watu wengi sana sasa asije akachafua hali ya hewa,”alisema.

“Kuna hupoteza fahamu,maisha, kuweka  rehani nyumba zao, mali zao kucheza kamari, na wanaliwa au kuna viongozi wengine wamewahi kutimuliwa madarakani kwa sababu ya kufungwa na Simba na Yanga.
Kwa hiyo, hii mechi ina mambo mengi sana, sasa sisi tunamuomba Akrama asiue watu, asifanye watu wakaliwa, asifanye watu wakapata mateso yasiyo na sababu,”alisema. 
“Pia mwamuzi akumbuke mechi inarushwa ‘live’ na SuperSport hivyo ambayo inaonekana duniani kote, hivyo kama akifanya vizuri itamsaidia kukuza taaluma yake na kupata ofa ya kuchezesha katika mechi ama mashindano makubwa,”aliongeza Kamwaga. 
Katika mchezo huo Akrama atasaidiwa na  Samuel Mpenzu kutoka Arusha na Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam wakati mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam. 
Kuhusiana na maandalizi ya mchezo huo, Kamwaga alisema kikosi chao kipo katika hali nzuri na cha kutia matumaini ni kwa mshambuliaji wao Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa akiugua Malaria kuanza mazoezi juzi hivyo kocha ndiye atakayeamua kama atampanga ama la. 
Kamwaga aliongeza kuwa wamejipanga kuendeleza ubabe kwa mahasimu wao hao kwa kuwafunga mabao mengi zaidi ya yale 5-0 waliyowafunga katika msimu uliopita wa ligi hiyo na kusema kuwa pamoja na kuwakosa nyota wao, Emmanuel Okwi na Amir Maftah katika mchezo huo hilo si tatizo. 
“Tuna silaha za maangamizi za kutosha ambazo kocha atazishusha  katika mchezo huo, hivyo tunatuma salamu kwa Yanga kwamba wasubiri zawadi nyingine ya mabao”,Alisema