Skip to main content

MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA TISA


Na Onesmo Ngowi


Masumbwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea………………………………….!

Afrika inahesabiwa kuwa na mabondia shapavu wanaotumika kuwapandisha chati mabondia wa nchi za Ulaya, Marekani na Asia. Kwa kuwa wengi wanatoka kwenye famililia za kipato cha chini hawana cha kufanya ila kuingia kwenye mtego huu na mwishoni wanaharibu rekodi na maisha yao kwa fedha ndogo.

Wapo mabondia toka Afrika ambao wameshatumika kuwapa mazoezi ya maandalizi mabondia kama kina Mike Tyson, Mumahhad Ali, Lenox Lewis, Evander Holyfield kwa malipo madogo sana. Mabondia hawa hulipwa kiasi kisichozidi dola 20 – 50 kwa kila raundi wanayocheza.

Lakini maumivu na madhara wanayopata ni sawa na kucheza pambano zima la raundi 8 – 12. Wakati wanalipwa dola 20 – 50 kwa raundi wenzao wanalipwa dola milioni 3 – 20 kwa pambano ambalo wakati mwingine huchukua kati ya dakika 1 – 20. Wengi wa mabondia hawa wamedhurika kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba hawawezi kuishi maisha ya kawaida na fedha za kujikimu hawana.

Nchi zinatakiwa kuweka sheria kali zinazowabana watu kuweza kuwatumia mabondia wake hovyo. Tusipofanya hivi tutaishia kuwa na vijana wengi walioharibika na walio mzigo kwetu sisi kama taifa.

Ni rahisi sana kwa kiongozi au mwananchi yeyote kupuuza jambo hili kwa madai kwamba “kwani ananihusu nini”. Lakini inapotokea kuwa na watu wengi walio na uharibifu wa ubongo na ambao hawawezi kujishughulisha na kazi za ujenzi wa taifa ni mzigo mkubwa kwa kila mwananchi.

Nchini Zambia walipata mzigo mkubwa sana kuwatunza kina Lottie Mwale na wengine ambao walikuwa hawawezi kujihudumia wenyewe. Taifa haliwezi kudharau kuwahudumia watu walioliletea sifa kemkem na matokeo yake wanahangaika kila siku kuwatunza.

Urahisi na njia za mkato kwa mabondia wa kitanzania kupelekwa nje ya nchi wengi kwa siri kutalipelekea taifa hili pabaya. Mabondia wengi wa kitanzania ama kwa urahisi wa kupata hati za usafiri au kwa msaada ya baadhi ya viongozi wa serikali wanasikika kucheza kila kona ya dunia.

Mengi ya mapambano haya wanadhulumiwa wengine wakirudimhawana hata pesa za nauli za kwenda kwao kutokea Dar-Es-Salaam.

Labda nieleze sababu kubwa ya TPBC kama msimamizi mkubwa wa taratibu, kanuni na sheria za ngumi za kulipwa hapa Tanzania, inapohahakisha kuwa bondia anatakiwa awe na vibali vyote kabla ya kwenda nje ya nchi.

1.         Usalama wa afya: TPBC hutaka kupata vielelezo vya afya ya bondia anayecheza na bondia wa Kitanzania
        ili kulinda afya ya bondia wetu asidhurike.
 
2.         Uwiano: TPBC hutaka kupata rekodi za bondia mpinzani ili ione kama bondia wa kitanzania hapigani na
        bondia mpinzani aliyemzidi sana ujuzi. Hili ni suala muhimu ili kulinda usalama wa bondia wa Kitanzania.
 
3.         Mkataba: ni lazima TPBC kuhakiki mkataba kwa ajili ya mambo yafuatayo:
 
(a)       Kuzuia kudhulumiwa.
 
(b)      Kuangalia vipengele vinavyoweza kumfunga bondia kwa promota. Mara nyingi mikataba ya ngumi ina
        vifungu vinavyomtaka bondia awe chini ya promota wa pambano kama atashinda, hivyo kumfunga kwenye
        mkataba huo. Mabondia wengi hawawezi kutafsiri hili na memeneja wengi huwaficha ukweli huu.
 
(c)  Mikataba mingi haifafanui faida nyingine bondia anazotakiwa kupata mbali na malipo ya pambano. Kwa
       mfano kama pambano husika linarushwa kwenye televisheni au linarusha matangazo, bondia anatakiwa alipwe
       asilimia kadhaa ya mapato haya mbali na fedha za pambano lenyewe. Hili ni suala la ufundi ambalo mabondia
       wengi hawajui na hivyo kupoteza haki zao kwa mameneja hawa waajabu.

Sisi tunao uwezo wa kusoma mkataba na kudai haki za bondia kabla ya pambano kwa kushirikiana na chama cha mchezo huo nchi unakochezwa. Lakini bondia anapotoroshwa na kurudi akilia baada ya kudhulumiwa (mara nyingi hutokea hata kutolipwa fedha hata senti tano) sisi kama Kamishrni hatuwezi kufanya lolote.
 
Kama nilivyokwisha eleza kwenye kurasa za mwanzo inakuwa rahisi sana kwa mameneja feki kuwapata mabondia kutokana na njaa zao kali. Mabondia wengi hawapati mapambano ya ngumi hivyo kukaa kwa muda mrefu na hawana njia nyingine ya kujipatia pato lolote mbali na kucheza ngumi. 
Wanapofuatwa na hawa mameneja feki kwao ni kama mungu kawaletea mkombozi (bila kujua kwamba ni kiama) hivyo wanakubaliana nao bila hata ya kuuliza maswala mengi mbali na fedha wanazopigania.
 Wengi hawana haja ya kujua wanacheza na bondia wa kiwango kipi, pambano ni la aina gani (ubingwa au lisilo la ubingwa). Wakishajua tu nchi wanayotakiwa kucheza, tarehe na uzito basi wanaingia kazini na kumwachia meneja kufanya mambo mengine muhimu. 
Muda wanaopewa kujiandaa ni mdogo sana hivyo maandalizi kuwa madogo sana sawa na kutoa jasho tu kwa wiki 2 au 3 kabla ya pambano. 
Wengi wao wakishapata tu uhakika wa kucheza huanza kukopa fedha za kujiandaa na imeshatokea mara nyingi kwa mabondia kuingia ulingoni kucheza na kulipwa fedha zote zinazoenda kulipa madeni waliyokopa na mara nyingi hata hazitoshi. Wanaporudi nyumbani huwa mikono mitupu.

Tabia hii haipo tu hapa kwetu Tanzania hata nchi kubwa kama Marekani na nchi za Ulaya zipo. Kuna mifano mngi ambayo bondia analazimika kucheza ili alipe madeni mbalimbali anayodaiwa kama fedha alizopoteza kwenye kamari, fedha za kuwatunza watoto anaodaiwa kuzaa na kina mama mbalimbali, madai ya kodi za serikali n.k. Huko Marekani mabondia wengi waliokwisha kuwa mabingwa wa dunia kama kina Roberto Duran na Mike Tyson wamo kwenye mkumbo huu.

Ni rahisi sana kwa bondia kuingia kwenye mkumbo huu kwani wakati akiwa kwenye chati anawaachia watu wengine kumeneji fedha zake. Watu hawa wanaoachiwa nao wana shida zao binafsi zinazohitaji fedha pia hivyo huzitumia kwa faida zao wenyewea.

Mabondia wengi mabingwa wa dunia waliopata kupeta sana waliishia kudaiwa mamilioni ya fedha baada ya kutoka kwenye chati. Wengi walikuta kwamba fedha zilizodaiwa kulipia kodi n.k. kazikutumika kwa malipo hayo hivyo kubakiwa na madeni makubwa ajabu.

Aidha ni kawaida kwa bondia kupoteza fedha nyingi kwenye matumizi ya kawaida. Kwa kuwa bondia ni shujaa kama nilivyokwisha sema hapo mwanzo ni mtu anayeheshimika na kupendwa. Daima huzungukwa na wapambe ambao hawaleti lolote mbali na kumla tu.

Naye kwa ajili ya kutunza sifa hawezi kuruhusu mtu yeyote (mpambe) ajigharamie mwenyewe. Watu wa kila aina wanaume kwa wanawake humzunguka na wengi wao wanayo malengo yao wanayotaka awatimizie au wanamtumia kuyatimiza.

Kazi nzito hutokea wakati chati ya bondia huyo inapofikia kikomo na kuanza kuona wapambe wake wakiyoyomea mmoja baada ya mwingine. Lakini kama bado anazo fedha watazidi kumzinga ili wazichangamkie. Wapambe ni watu wa kwanza kabisa kujua wakati fedha zinapoishia kabla hata ya mhusika mwenyewe.

Wapambe wana pua ndefu zinazonusa mifuko kuanzia chini kabisa. Kitu rahisi kabisa kwao kuanza kuona ni wakati mtirirko wa huduma unapopungua. Kama ni wanywaji waliokuwa wanakunywa bia 20 kwa siku inapofikia kuambulia chupa 10 basi wanaanza kujiandaa kutimka.

Lakini wapambe ni watu wasio na faida yoyote mbali na kukaa tu kumsifia bondia na kumdanganya kwamba hakuna mtu mwingine kama yeye. Ili wamle vizuri wengine wanadiriki hata kumfananisha na Rais wa nchi.  Wapo wanaoenda mbali na kumfananisha bondia wanayemla na watakatifu fulani.

Bondia anapoisha na kwa bahati mbaya awe hakuwekeza fedha zake au anao ujuzi mwingine mbali na ngumi basi huishia mahala pabaya sana. Wapo wanaoishia kuwa walinzi (korokoroni), madobi, mabaunza, makuli na fani za kila aina.

Ninilisema hapo mwanzo kuwa elimu ndogo ndilo tatizo kubwa la mabondia wetu. Kwa kukosa elimu inayoweza kuwapa ujuzi mbalimbali wanapoisha kimchezo basi inakuwa ndio mwisho wao. Nataka nieleze wazi kuwa tatizo hili sio hapa kwetu Tanzania peke yake.

Hata nchi zilizoendelea pia wana tatizo hili. Tofauti ya wenzetu ni kwamba wakati bondia akiwa kwenye chati huingizwa kwenye mifuko mbalimbali ya Pensheni na akiba hivyo baada ya kutoka kwenye chati basi wanaendelea kulipwa fedha za mafao.

Japokuwa wapambe ndo basi tena lakini angalao wana fedha za kujikimu. Vile vile utakuta wanawekeza fedha kwenye bima mbalimbali au makampuni mbalimbali ya biashara yanayowapa faida kila baada ya vipindi kadhaa. Mfumo huo hapa kwetu Tanzania bado hakuna.

Lakini ni muhimu kuweko na sheria zinazowataka wanamichezo wetu kuwekeza fedha zao kwa kujiunga na mifuko mbalimbali ya Pensheni. Tusipofaya hivyo tutaishia kuwa na ma-stars wetu waliong’ara duniani kama mabaunsa, walinzi, madobi na hata makuli.

Ni wazi kwamba watakuwa sio mifano ya kuigwa kwenye jamii hata kidogo. Hii inadidimiza sana michezo (kwani hakuna mzazi atakayediriki kumwachia mwanae ajiunge na michezo kwa hofu ya kuwaona kwenye hali mbaya).

Lazima kuwe na mifumo itakayobadilisha kabisa maisha ya wanamichezo wetu, hata kama itabidi serikali kutumia gharama kubwa kuiweka mifumo hii. Kwa hali ya sasa ni vigumu kwa Watanzania wengi kujitokeza kujiunga na michezo kama ajira kwani hakuna watu wengi wa kuigwa. Tungekuwa na wanamichezo wenye mafanikio na wanaoendesha maisha yao vizuri basi karibu kila Mtanzania angejiunga na michezo.

Watokee tu wanamichezo 10 wanaomiliki Benzi jijini Dar-Es-Salaam basi kila mtu anagejiunga na michezo.Inaendelea…………..!
 
Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com