SIMBA YAANZA KUTETEA UBINGWA LIGI KUU LEO

Mabingwa watetezi, Simba SC wanaanza na African Lyon leo
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaanza leo kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja saba tofauti, kuwania pointi za kuanza vema msimu mpya.
Mabingwa watetezi Simba wataikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mjini Morogoro, Polisi Dodoma watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati jijini Tanga, Mgambo JKT ambayo imepanda daraja msimu huu itaumana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Tanzania Prisons ambayo nayo imerejea VPL msimu huu itaialika Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. JKT Ruvu na Ruvu Shooting zitapambana kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam huku Azam ikiwatembelea Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Katiba.
Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans dhidi ya Oljoro JKT. Mechi zote zitaanza saa 10.30 jioni.
Wakati msimu huo unaanza leo, bado Simba, ambao ni mabingwa watetezi, Azam washindi wa pili na Yanga washindi wa tatu zinapewa nafasi kubwa ya kuendelea kutawala kwenye ligi hiyo- kwa kifupi Ligi Kuu itakuwa mbio za farasi watatu, wengine wanatarajiwa kuwa wasindikizaji.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Mserbia Boris Bunjak amesema timu yake ipo tayari kwa Ligi Kuu, lakini tu amehadharisha marefa wachezeshe kwa haki.
Bunjak alikerwa mno na marefa waliochezesha mechi ya Ngao ya Jamii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi kwamba waliwabeba wapinzani wao Simba SC.
Mechi hiyo ilichezeshwa na Martin Sanya, aliyeisaidiwa na Omar Kambangwa na Ephron Ndissa, wakati refa wa akiba alikuwa Oden Mbaga na Kamisaa Omary Kasinde.
Bunjak alisema kwamba marefa hao walionyesha mapungufu makubwa kwa kuwapendelea wazi wazi Simba na hata wakafanikiwa kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.
“Nafikiri tulicheza mechi nzuri, tukaongoza 2-0, baada ya hapo tukapoteza nafasi nzuri za kufunga, lakini siamini kwa nini refa alitoa penalti dakika ya mwisho(kipindi cha kwanza), kwa sababu ule mpira ulikuwa kwenye himaya ya wachezaji watatu kutoka nyuma, unaweza kuonaje nani aliucheza kwa mkono.
Bao la pili, pia ulikuwa msaada mkubwa, niliandaa timu yangu kucheza dhidi ya wachezaji 10, siyo wachezaji zaidi, mimi si kocha nayeandaa timu kucheza dhidi ya wachezaji wengi, naweza kufanya nini, tulicheza vizuri, tulipoteza nafasi, refa alitunyima penalti mbili, asilimia 100, naweza kufanya nini, labda hii ni soka ya Tanzania tu.
Nitafanya nini, huu ni uzoefu wangu wa kwanza ofisini tena, lakini nimeshangazwa sana, Simba ni timu kubwa, Simba ni timu nzuri, lakini leo Azam imecheza vizuri, Azam ilistahili kushinda taji,”alisema.
Kocha huyo alionyeshwa kuridhishwa na bao moja tu la Simba, la tatu ambalo alisita kulizungumzia kabisa katika malalamiko yake.
Nayo Simba, inayofundishwa na Mserbia Profesa Milovan Cirkovick, itashuka dimbani kumenyana na Lyon, ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC na kutwaa Ngao ya Jamii, kwa mara ya pili mfululizo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumanne wiki hii.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kwamba mechi dhidi ya Prisons itakuwa ngumu kwa sababu anaamini wapinzani wao watakamia na watasaidiwa na kucheza nyumbani.
Lakini pia, Saintfiet alisema Prisons haina presha ya kufungwa na Yanga kwa sababu ni timu kubwa, hivyo watacheza kwa utulivu, wakipata sare ni safi, wakifungwa hakuna tatizo na wakishinda kwao itakuwa ‘sikukuu’.
Mtakatifu Tom ametua Mbeya na wachezaji 22 kwa ajili ya mechi hiyo ambao ni makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan,  Nadir Haroub ‘Cannavaro’, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika, viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nizar khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva na washambuliaji ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza.