KIKOSI cha timu ya Yanga kimeingia
kambini jana katika Hotel ya Uplands iliyopo Changanyikeni jijini Dar es Salaam
kujiandaa na mechi yake dhidi ya mahasimu wao Simba itakayopigwa Oktoba 3,
kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya
klabu hiyo jana zinaeleza uongozi umefikia hatua ya kuweka kambi kutokana na utulivu iliopo eneo hilo
wakiamini wachezaji watapata wasaa mzuri wa kujiandaa na mechi hiyo
itakayochezwa Jumatano.
Kabla ya kucheza na Simba, Yanga
inayojifua kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, keshokutwa itakuwa
kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kucheza na African Lyon.
Yanga yenye pointi nne ilizovuna kwenye
mechi tatu ilizocheza tangu kwanza kwa ligi hiyo Septemba 15, Jumapili hii
itakuwa ikipigania ushindi kwa Lyon kujiweka fiti kisaikolojia pia kufikisha
pointi saba kabla ya kucheza na Simba.
Aidha, Yanga chini ya Kaimu Kocha Mkuu
wake Fred Felix Minziro, itawakabili Simba wakikumbuka kisago cha mabao 5-0,
walichopata katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya msimu uliopita ambayo
ilihitimishwa Mei 6.
Kwa kutambua umuhimu wa pointi tatu
katika mechi hiyo ya watani wa jadi, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji
aliyeingia madarakani Julai 15, ametoa sh milioni 100, kuamsha hamasa ya
maandalizi kwa wanachama kuelekea mechi hiyo.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya klabu hiyo
kimedokeza kuwa, Manji ametoa fedha hizo kuamsha hamasa kwa ajili ya kuisapoti
timu yao wakati wote wa mechi na kuhakikisha wanaibuka na ushindi
ili kupata ponti tatu na kurejesha
heshima ya klabu hiyo.
Yanga iliyoanza ligi hiyo kwa sare ya
bila kufungana na Prisons kabla ya kufungwa 3-0 na Mtibwa Sugar, ilizindukia
kwa JKT Ruvu kwa kuinyuka 4-1, huku Simba ikiwa na rekodi ya kushinda asilimi
10, ikishinda mechi zote tatu.
Wakati Yanga itakutana na Simba ikitoka
kucheza na Lyon, mabingwa watetezi Simba ambao wamejichimbia visiwani Zanzibar,
watakutana na wakali hao wa Jangwani wakitokea kucheza na Tanzania Prisons ya
Mbeya, mechi itakayochezwa kesho Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Aidha, wakati Simba chini ya kocha wake
Mserbia, Milovan Cirkovic siku hiyo itaikabili Yanga bila nyota wake wa
kimataifa Mganda, Emmanuel OKwi, Yanga wao watakuwa bila Kocha Mkuu wake, Mbelgiji
Tom Saintfiet, aliyetimuliwa.
Saintfiet aliyetua Jangwani Julai 4 na
kusaini mkataba wa miaka minne, mkataba wake ulisitishwa hivi karibuni kutokana
na sababu kadha wa kadha, hivyo Minziro kushikilia mikoba hiyo kwa muda, wakati
uongozi ukisaka wa kuziba nafasi.
Comments
Post a Comment