JESHI LA YANGA SC LAZIDI KUIMARIKAMABINGWA wa Afrika Mashariki na Kati, ‘Kagame Cup’ Yanga, wamezidi kuimarika baada ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi akiwemo kiungo  Nurdin Bakari kuanza mazoezi jana.
Nurdin ambaye alikuwa nje ya dimba kwa muda mrefu, baada ya kuumia akiwa na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, jana aliungana na wenzake katika mazoezi ya asubuhi kwenye uwanja wa Sekondari ya Loyola, ikiwa ni maandalizi ya Ligi Kuu Bara itakayoanza Septemba 15.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa mbali na Nurdin, viungo Rashid Gumbo na Athuman Iddi ‘Chuji’ ambao walikuwa na malaria, nao waliungana na wenzao jana katika mazoezi.
Hata hivyo, Sendeu alisema, kipa wao namba tatu, Said Mohamed, ambaye naye alikuwa anaugua malaria, hali yake bado haijatengemaa.
“Naweza kusema kwa kiasi kikubwa kikosi cha Yanga kipo kamili, baada ya wachezaji waliokuwa wagonjwa kuanza mazoezi…kwa sasa anayekosekana kundini ni Mganda Hamis Kiiza tu, ambaye yupo kwao akiitumikia timu ya taifa”, aliongeza Sendeu.
Yanga itaanza ligi hiyo kwa kucheza ugenini dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye dimba la Sokoine.