SIMBA YATOA ONYO KWA WANACHAMA WATAKAOVURUGA MKUTANO J'2


MKUTANO Mkuu wa Wanachama Wote wa Simba utafanyika Agosti tano mwaka huu katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay kama ilivyopangwa.
Mipango yote kwa ajili ya mkutano huo muhimu kikatiba imekamilika na klabu inawaomba wanachama wake wote hai kuhudhuria mkutano huo muhimu.
Uongozi umepanga kutoa mabasi kwa ajili ya kuwasafirisha wanachama wake kutoka katika maeneo mbalimbali kwenda katika ukumbi wa mikutano.
Kutakuwa na mabasi matatu kwenye eneo la Shibam Magomeni... Mabasi matatu Temeke mwisho na mabasi matatu katika makao makuu ya Simba SC Mtaa wa Msimbazi.
Pia klabu itapeleka mabasi mawili katika wilaya za Mkuranga na Kibaha kwa ajili ya kuwaleta wanachama wake walio katika mkoa wa Pwani kuhudhuria mkutano huo.
Mwenyekiti wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, amewahakikishia wanachama wa Simba kwamba mkutano huo utaendeshwa kisasa na usalama umehakikishwa kwa asilimia 100 kwa vile eneo la mkutano liko chini ya Jeshi la Polisi.
"Napenda kuwahakikishia wanachama wote wa Simba kwamba mkutano huo utakuwa bora na wote watakaokuja watafurahi na kujisikia fahari kuwa washabiki wa klabu ya soka ya Simba. Kwa wale ambao wamepanga kuja kufanya vurugu kwenye mkutano huo, klabu itaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake," alisema.