SIMBA YALAMBWA 3-1 NA CITY STARS SIMBA DAY


Wachezaji wa Simba walioanza


Walioanzia benchi
 Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC imefungwa mabao 3-1 na Nairobi City Stars katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana katika mechi iliyochezwa sambamba na Simba Day.
Lakini kufungwa huko kwa Simba kulitokana na kocha Milovan Cirkovick kubadilisha karibu kikosi kizima kilichoanza na kuingiza wachezaji wapya, ambao waliitoa City Stars ya Nairobi nyuma kwa 1-0 na kuipa ushindi wa 3-1.
Simba ilitangulia kupata bao kupitia kwa Felix Sunzu dakika ya 15, pasi ya Mwinyi Kazimot na ilikwenda kupiumzika ikiwa mbele kwa bao hilo.
Lakini kipindi cha pili, kipa aliyempokea Juma Kaseja, Hamadi Waziri alitunguliwa mabao matatu katika dakika 57 na Duncan Owiti, dakika ya 64 na Bruno Okullu na dakika ya 79 na Boniphace Onyango.  
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Simba, Milovan alisema kwamba alibadilisha kikosi kizima kipindi cha pili, kwa sababu alitaka awaone wachezaji wote uwezo wao.
Alipoulizwa kuhusu muda uliobaki kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanza, kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam mwishoni mwa mwezi huu, Milo alisema muda unatosha na atakuwa kikosi tishio.
“Nina wachezaji wazuri wengi, hujamuona Kapombe uwanjani leo, muda unatosha sana,”alisema Milovan, raia wa Serbia.
Mapema katika tamasha hilo, Simba ilitoa tuzo mbalimbali kwa wachezaji wa sasa na wa zamani kwa mchango wao kwenye klabu hiyo, pamoja na baadhi ya wadau wake.
Waliopewa tuzo kwa wachezaji wa sasa, ni Shomary Kapombe (Nidhamu), Emmanuel Okwi (Mchezaji bora wa msimu) na marehemu Patrick Mfisango (Heshima).
Wa zamani ni Haidari Abeid ‘Muchacho’ (Mchezaji Bora miaka ya 1970), Hamisi Kilomoni (Mchezaji Bora Miaka ya 1960), Ally Sykes (Heshima, Udhamini), Profesa Philemon Sarungi (Mchango wa muda mrefu klabuni) na Gaorge Kavishe, Meneja wa Kilimanjaro Beer, Wadhamini wa sasa wa Simba SC.
Katika mechi ya kwanza, timu na wanawake ya Simba, Simba Queens, iliifunga Ever Green ya Temeke mabao 5-3 katika mchezo wa Ligi ya Wanawake, Dar es Salaam uliokwenda sambamba na tamasha la Simba Day, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Simba alikuwa ni Maimuma Hamisi ‘Ronaldo’ aliyefunga mabao matatu, katika dakika za tano, 62 na 64, wakati mabao mengine ya Malkia wa Msimbazi, walio chini ya kocha Anthony Makunja, yalifungwa na Grace Tony dakika ya 48 na Neema Kuga dakika ya 59.
Mabao ya Ever Green yalifungwa na Sherida Boniface dakika ya 53, Vumilia Maarifa dakika ya 55 na Amina Siraj dakika ya 61.

SOURCE: http://bongostaz.blogspot.com