MORO UNITED YAPANIA KUREJEA LIGI KUU BARA


UONGOZI wa klabu ya Moro United umeweka mikakati ya kuhakikisha timu hiyo inashiriki vema ligi daraja la kwanza na hatimaye kurejea tena katika ligi kuu soka Tanzania Bara.
 Mwenyekiti wa timu hiyo Rodgers Peter alisema kwamba katika kuhakikisha hilo linatimia wameona waziungatie zaidi katika kusajili kikosi ambacho  kitashiriki kikamilifu ligi hiyo itakayoshirikisha timu 24.
Alisema usajili wao umezingatia wachezaji chipukizi zaidi na wenye vipaji vya hali ya juu hali itakayowafanya waweze kukaa kwa muda mrefu na hivyo kuifanya timu kuwa na umoja.
“Yaani tumedhamiria kurejea katika ligi kuu bara, tumehakikisa tunasajili wachezaji chipukizi ili tuwe nao kwa muda mrefu na timu iweze kucheza kitimu hasa, pia tumeangalia kipaji binafsi na uwezo wa kuhimili mikiki mikiki ya uwanjani”, alisema Rodgers.
Rodgers aliongeza kuwa, kikosi cha timu hiyo kinaendelea na mazoezi yake ya kujiandaa na ligi hiyo katikia uwanja wa Kwa Bibi uliopo Tabata Segerea chini ya kocha wake Mkuu, Yussuf Macho ‘Musso’.
Alisema, pamoja na mazoezi yake timu yake inacheza mechi mbalimbali za kirafiki ambazo zinamsaidia kocha wao kujua kiwango cha wachezaji wake na kama kuna mapungufu ili aweze kuyafanyia marekebisho kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.