MICHUANO BANC ABC SUP8R KUENDELEA LEO


Mechi za michuano ya BancABC SUP8R inayoshirikisha timu nane bora kutoka Tanzania Bara na Zanzibar zinaendelea leo kwenye miji ya Dar es Salaam, Moshi, Mwanza na Zanzibar. 
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Saad Kawemba na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) chini ya Rais wao Amani Makungu walikutana jana mjini Zanzibar kuzungumzia maendeleo ya michuano hiyo. Viongozi wengine wa ZFA waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu Kassim Haji Salum na wajumbe saba wa Kamati ya Utendaji. 
Katika kundi A Jamhuri itacheza na Zimamoto kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuanzia saa 2 kamili usiku, wakati Simba itaparurana na Mtende kwenye Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi. Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni. 
Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza utakuwa mwenyeji wa mechi ya Polisi Morogoro na Super Falcon. Mechi hizo zote za kundi B zitaanza saa 10 kamili jioni.
 Hatua hiyo ya makundi itamalizika Agosti 12 mwaka huu kwa mechi nne. Simba na Zimamoto zitaoneshana kazi Uwanja wa CCM Kirumba wakati Jamhuri na Mtende zitacheza kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. 
Mechi za kundi B zitakuwa kati ya Super Falcon na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan na Azam dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Ushirika.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)