JESHI LA MAUAJI SIMBA SC HILI HAPA


Ochieng na Akuffo

WAKATI jana zoezi la kuwasilisha usajili wa wachezaji wa vilabu vya Ligi Kuu soka Tanzania Bara na timu za vijana, mabingwa wa ligi hiyo Simba, wamefunga usajili wao kwa kuwaweka wachezaji wawili wa kimataifa, Mghana Danniel Akuffo na Mkenya Pascal Ochieng. 
Aidha, Simba inatarajia kupokea mchezaji wa kimataifa kutoka nchini Mali , Abdul Azizi ambaye ataletwa na wakala wa wachezaji Vaier St.Claire na Simba itaagalia jinsi gani itamfanyia mchezaji huyo kwani zoezi limeshafungwa. 
Simba ambayo jana iliwatambulisha wachezaji hao wapya kwa waandishi wa habari, imewasilisha pia majina ya Emmanuel Okwi, Mussa Mudde na Felix Mumba Sunzu hivyo kufikisha wachezaji watano wa kimataifa wanaohitajika kusajiliwa kwa mujibu wa kanuni. 
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema jana kwamba wamemsajili Akuffo kwa mwaka mmoja baada ya wakala wake kuwaeleza kuwa nyota huyo yupo katika mpango wa kwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa mwakani. 
Alisema wachezaji hao wanatarajiwa kushuka dimbani na kikosi cha Simba kitakachokwaana na AFC Leopards keshokutwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, pia watakuwepo katika mechi ya ngao ya jamii baina Azam itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .
 Alisema mbali na hao, katika usajili wao wamewasilisha majina ya wachezaji wake Kelvin Yondan aliyesajiliwa Yanga na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ waliomsajili kutoka Azam Fc na kusema kuwa suala la wachezaji hao litamalizwa na kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). 
Yondan ambaye alizua utata baada ya kumwaga wino kuichezea Yanga huku Simba ikidai kuwa bado inamkataba naye, jina lake pia limeorodheshwa na Yanga katika usajili wa wachezaji watakaoichezea timu hiyo katika msimu wa 20012/2013.
 “Suala la Redondo nalo pia litashughulikiwa TFF kwani Simba tumejitahidi kuwa waungwana katika hili na kufanya mazungumzo na Azam ambayo bado hayajawa mazuri…lakini mchezaji mwenyewe anadai hana mkataba sasa TFF ndiyo itajua nani mkweli na nani muongo,”aliongeza Kamwaga. 
Wachezaji wengine waliojumushwa kwenye usajili wa Simba ni pamoja na Juma Kaseja, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Nassoro Said Cholo, Amir Maftah, Juma Nyoso, Uhuru Seleman, Haruna MOshi ‘Boban’, Paul Ngalema na Abdallah Juma. 
Wengine ni Hamad Waziri Mwinyimani, Salum Kinje, Mrisho Ngassa,  Haruna Shamte, Jonas Mkude, Edward Christopher, Shomary Kapombe, Haruni A.Chanongo, Omary Seseme, Hassan Kondo na Kiggi Makasi.