HATIMAYE TWITE AUNGANA NA YANGA RWANDA


BEKI wa kimataifa wa mabingwa wa klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’ Yanga,  Mbuyi Twite amejiunga na kikosi cha timu hiyo kilichopo  nchini Rwanda.
 Twite ambaye ameziingiza katika msigano timu za Simba na Yanga baada ya kusaini mkataba katika vilabu hivyo akianza Simba na baadaye Yanga ambayo pia imeliwasilisha jina lake katika usajili wa wachezaji katika shirikisho la Soka Tanzania (TFF) alikuwa kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa ajili ya kuiaga familia yake.
 Akizungumza  kwa simu kutoka Kigali nchini Rwanda, Mjumbe wa kamati ya Utendaji ya Yanga Abdallah Binkleb alisema kwamba Twite aliwasili huko jana na leo asubuhi alifanya mazoezi na wenzake katika uwanja wa Amahoro.
 Alisema kama mambo yakienda vema huenda nyota huyo aliyesajiliwa kutoka APR ya huko kesho atashuka  katika dimba la Amahoro akiwa ametinga uzi wa njano na kijani katika mchezo wao na Rayon utakaopigwa jioni.