SIMBA YAIRARUA PORTS 3-0

Kikosi cha Simba leo; Picha kwa hisani ya http/bongostaz.blogspot.com 
Na Prince Akbar
MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC leo ni kama wamekata tiketi ya kuingia Robo Fainali Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kuichapa Ports ya Djibouti mabao 3-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Simba leo, alikuwa mshambuliaji mpya kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, Abdallah Juma aliyeingia kuchukua nafasi ya Amri Kiemba mwanzoni mwa kipindi cha pili aliyefunga mabao mawili dakika za 60 na 73 na Felix Mumba Sunzu Jr. aliyefunga moja kwa penalti dakika ya 64  
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila nyavu za Ports kutikisika, na katika kipindi hicho Sunzu, mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, alipoteza nafasi tatu za wazi mno, za kufunga mabao akiwa amebaki yeye na kipa, Kalid Ali Moursal.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mserbia, Milovan Cirkovick kipindi cha pili kuwaingiza Juma Nyosso kuchukua nafasi ya Haruna Shamte, Abdallah Juma aliyechukua nafasi ya Kiemba na baadaye Uhuru Suleiman kuchukua nafasi ya Haruna Moshi ‘Boban’ yaliisaidia Simba.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi tatu baada ya kucheza mechi mbili na sasa inashika nafasi ya tatu kwenye Kundi A, nyuma ya URA yenye pointi sita na AS Vita yenye pointi tatu na wastani mzuri wa mabao. Simba itamaliza na AS Vita ya DRC, mechi ambayo itakuwa kali kwa sababu timu zote zina pointi sawa.   
Simba SC; Juma Kaseja, Haruna Shamte/Juma Nyosso, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Haruna Moshi ‘Boban’/Uhuru Suleiman, Mussa Mudde, Felix Sunzu, Amri Kiemba/Abdallah Juma, Mwinyi Kazimoto, Lino Masombo na Kanu Mbivayanga.
Porst FC; Kalid Ali Moursal, Kadar Abass Abanel, Mohamed Omar Arab, Abdourahman Isman, Jean Paul Niyobabariba,  Mehdi Ahmaed Moumin, Vincent Taboko Agbor, Omar Mohamed Hassan/ Ryad Said Awad., Daher Hassan Ali, Roland Ayuk Agbor na Gasama Jean Bosco/ Abdillahi Hamadou.
katika mchezo uliotangulia wa kundi hilo, URA ya Uganda, ilikuwa timu ya kwanza kufuzu Robo Fainali ya baada ya kuichapa mabao 3-1, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
Mabao ya URA yaliwekwa kimiani na Sula Bagala mawili na Robert Ssentongo, wakati la kufutia machozi la Vita, inayofundishwa na kocha w zamani wa Yanga, Raul Jean Pierre Shungu lilifungwa na Mutombo Kazadi.
 
MSIMAMO WA KUNDI A

                     P   W  D  L   GF      GA     GD     Pts
URA             2   2   -    -    5         1         4         6
AS Vita        2   1   -    1   8         3         5         3       
Simba           2   1   -    1   3         2         1         3
Ports             2   -    -    2   -         7         -7       -

SOURCE: BIN ZUBEIRY (http/bongostaz.blogspot.com)