SIMBA, AZAM 1-1 URAFIKI ZANZIBAR

Humud alipewa kadi nyekundu mapemaa, 
lakini Simba hawakutumia nafasi

Na Prince Akbar
MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC usiku huu wameshindwa kuwafunga washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam FC licha ya kucheza pungufu katika mchezo wa Kundi A wa Kombe la Urafiki, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, baada ya kutoka sare ya 1-1.
Simba ilitangulia kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake iliyemsajili kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam, Danny Mrwanda, lakini Azam ilisawazisha kupitia kwa George Odhiambo ‘Blackberry’ dakika ya 45.
Abdulhalim Humud alipewa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu dakika ya 52 na kutolewa nje, hivyo Azam kubaki pungufu ya mchezaji mmoja uwanjani.
Katika mechi yake ya kwanza juzi, Simba SC ilianza vyema baada ya kuifunga Mafunzo mabao 2-1, wakati Azam ililazimishwa sare ya 1-1 na U23, Karume Boys.
Simba sasa inaongoza kundi hilo kwa pointi zake nne, mabao matatu ya kufunga na mawili ya kufungwa, wakati Azam FC ni ya pili kwa pointi zake mbili  
Simba; Juma Kaseja, Haruna Shamte, Paul Ngalema, Lino Masombo, Shomary Kapombe, Amri Kiemba/Edward Chirtopher, Mwinyi Kazimoto/Salim Kinje, Mussa Mudde/Jonas Mkude, Abdallah Juma, Kanu Mbivayanga/ Uhuru Suleiman na Danny Mrwanda/Abdallah Seseme.
Azam: Deo Munishi ‘Dida’, Samir Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Said Mourad, Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Kipre Herman Tcheche, Kipre Michael Balou, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Gaudence Mwaikimba na George Odhiambo ‘Blackberry’/Hamisi Mcha.
Katika mchezo wa awali wa kundi hilo jioni ya leo, Karume Boys ilishinda 1-0 dhidi ya Mafunzo, bao pekee la Nassor matter dakika ya 45.
Aidha, mapema jioni ya leo, Yanga ilirudishwa nyumbani Dar es Salaam, kwa kitendo cha kupeleka timu B badala ya timu A.
Yanga ilikuwa Kundi B pamoja na Jamhuri, Falcon na All Stars. Jana ilifungwa 3-2 na Jamhuri katika mchezo wao wa kwanza