MWAKALEBELA CUP KUANZA JULAI 7


MICHUANO ya Kombe la Mwakalebela, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi mjini Iringa, kuanzia Julai saba, huku ikishirikisha michezo ya Netiboli  na mpira wa Miguu kwa timu za Iringa mjini.
Michuano hiyo ni muendelezo wa kuendeleza michezo kwa mdau wa michezo, Fredrick Mwakalebela (pichani), aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwakalebela, alisema kwamba kwa netiboli, timu za kwenye kata 16 zitashiriki.
Alisema kwamba anaamini kwa kuanzisha michuano hiyo,mambo  yatakuwa mazuri na kuwafanya wanamichezo kujiweka katika ramani nzuri kimichezo.
Lengo langu ni kufanya wanamichezo wajiweke katika kiwango cha juu,hivyo naamini huu ni wakati wao vijana kufanya kazi ya maana.
Naamini kila siku kinachotakiwa kufanywa ni kuwekeza katika michezo, hivyo lengo halisi litajulikana na kuendeleza michezo mkoani Iringa na Tanzania kwa ujumla,” alisema Mwakalebela.
Kata ambazo zitachuana kwa timu za wanawake za netiboli ni pamoja na Ruaha, Kigonzila, Mshindo, Mwangata, Gongilonga na nyinginezo zinazounda jimbo la Iringa Mjini.
Aidha katika timu zinazotarajiwa kushiriki katika michuano hiyo ya Mwakalebela Cup ni pamoja na Lipuli, African Wonders na nyinginezo zilizosheheni wanamichezo wenye uwezo wa juu.
Mwakalebela ni miongoni mwa wadau makini w2a mpira wa miguu,huku akikumbukwa na wengi kwa utendaji kazi wake mzuri na uliochangia kwa kiasi kikubwa kukuza mpira wa miguu.
Baada ya kumaliza kipindi cha uongozi wa TFF, Mwakalebela, alikwenda kuwania ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM, hata hivyo alienguliwa na chama chake.