SIMBA, WAGANDA SASA KUCHEZA JUMAPILI


Mechi ya Simba na URA ya Uganda kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) iliyokuwa ichezwe Jumatatu (Julai 16 mwaka huu) sasa itafanyika Jumapili (Julai 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limefanya mabadiliko hayo kutokana na fainali ya Copa Coca-Cola 2012 iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo kuhamishiwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. 
Kutokana na mabadiliko hayo, mbali ya mechi ya Simba na URA itakayoanza saa 10 kamili jioni, mechi nyingine Jumapili itakuwa kati ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) dhidi ya Ports ya Djibouti itachezwa saa 8 kamili mchana Uwanja wa Chamazi. 
Pia siku hiyo hiyo ya Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi nyingine itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi hiyo itazikutanisha timu za Azam ya Tanzania Bara na Mafunzo kutoka Zanzibar. 
Mechi za ufunguzi wa mashindano hayo Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitabaki kama zilivyopangwa awali. Mechi ya kwanza saa 8 mchana itakuwa kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya Sudan Kusini wakati saa 10 kamili jioni Yanga itaoneshana kazi na Atletico ya Burundi.

Comments