ULAYA KWAMKOSESHA OKWI KAGAME


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba Mganda Emmanuel Okwi hatoshiriki na timu yake katika michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama ‘Kombe la Kagame’ inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 14 jijini Dar es Salaam.
Simba itaanza michuano hiyo julai 16 kwa kukwaana na URA ya Uganda, mchezo utakaopigwa kuanzia saa 10.00 jioni kwenye uwanja wa Taifa.
Okwi atakosa michuano hiyo kufuatia nyota huyo kupata ofa ya kufanya majaribio katika vilabu tofauti nje ya nchi ambapo atautumia mwezi huo katika zoezi hilo.
Kiongozi mmoja wa Simba amesema leo kwamba Okwi anatarajia kuanza safari yake ya majaribio Julai 4 ambapo ataelekea nchini Italia.
Alisema kuwa mbali na Itali, nyota huyo anayekipiga pia timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ amepata ofa ya kucheza nchini Ujerumani na Poland.
“Kama hatofuzu majaribio nchini Italy atakwenda Ujerumani ambapo kuna timu moja imemtaka afanyiwe vipimo tu na kujiunga…kama vipi atakwenda Poland kazi imebaki kwake kuamua,”alisema kiongozi huyo.
Aidha, Simba inaendelea na maandalizi yake ya michuano ya Kagame ambapo kesho itashuka katika dimba la Taifa kukipiga na mabingwa wa Uganda, Express.
Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema leo kwamba maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekamilika ambapo Simba itashusha nyota wake wapya iliyowasajili sambamba na wale wa zamani.
Alisema mchezo huo ni muhimu kwao kwani kocha ataweza kujua kiwango ilichofikia kikosi chake ambacho kimekuwa kikijinoa kwa majuma kadhaa.
Kamwaga aliongeza kuwa timu hiyo itaelekea Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kambi maalum sambamba na kushiriki kombe la Tanzania ‘Urafiki’ lililoanza kutimua vumbi jana. 
Jumla ya timu nane zitashiriki katika michuano hiyo ambapo Simba ipo kundi A pamoja na  Azam, Mafunzo na timu ya soka ya taifa ya vijana ya Zanzibar wenye umri wa chini ya miaka 23 (Karume Boys) ambapo itaanza michuano kesho usiku kwa kucheza na Mafunzo ya Zanzibar .

Comments