TOVUTI YA KANDANDA GALACHA YAJITOSA TUZO ZA MWANAMICHEZO BORA WA TASWA 2012


TOVUTI ya Kandanda.galacha.com ya jijini Dar es Salaam imejitosa kudhamini Tuzo za Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2011 upande wa soka.
Wakizungumza kwenye mkutano na waandishiwa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa tovuti hiyo, ambayo pia ina tovuti nyingine iitwayo kandanda.co.tz, Erick Zomboko alisema tovuti yao inahusiana na masuala ya mpira wa miguu na wameona wajiunge katika hatua ya kuendeleza michezo hapa nchini.
Alisema wanathamini tuzo hizo zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), hivyo pamoja na upya wao katika masuala ya tasni ya habari wameona waunganishe nguvu kusaidiana na TASWA.
Alisema katika udhamini wao watatoa tuzo maalum kwa washindi upande wa mpira wa miguu na pia watatoa fedha taslimu kwa washindi hao, lakini hawawezi kutangaza kiasi cha fedha watakachowapa washindi hadi siku hiyo.
Zomboko alitaja watakaowania tuzo hiyo kuwa ni wale waliotangazwa na Kamati ya Tuzo upande wa mpira wa miguu kwa wanaume, ambao ni Juma Kaseja (Simba), Aggrey Morris na John Bocco wote wa Azam, wakati mpira wa miguu wanawake ni Fatuma Mustapha (Sayari),  Ito Mlenzi (JKT), Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ na Asha Rashid ‘Mwalala’ wote wa timu ya Mburahati Queens.
Wachezaji wengine ambao watawania tuzo hiyo ni wale wa nje wanaocheza soka Tanzania, ambao ni Haruna Niyonzima (Yanga), Emmanuel Okwi (Simba) na Kipre Tchetche (Azam).
“Haya ni makundi matatu tofauti, ambayo yametangazwa na Kamati ya Tuzo ya TASWA, tutakachofanya sisi mshindi wa kila kundi tutampa zawadi yake siku hiyo ya sherehe, itakuwa ni tuzo pamoja na kiasi fulani cha fedha, tuzo ambayo itakuwa na jina la mhusika,” alisema na kuongeza kuwa udhamini huo ni kiasi cha sh. Milioni sita.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa TASWA inayoandaa tuzo hizo, Maulid kitenge aliishukuru tovuti hiyo na kusema licha ya kwamba wana udhamini wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, lakini bado hautoshi, hivyo wadau mbalimbali wanakaribishwa kuwaunga mkono katika juhudi zao za kuwatuza wanamichezo.
Sherehe za kuwazawadia Wanamichezo Bora wa Tanzania zinatarajiwa kufanyika Alhamisi wiki hii ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, ambapo michezo mbalimbali itazawadiwa.
Wakati huohuo, Kitenge alisema Jumatatu saa tano asubuhi TASWA wanataraji kufanya mkutano na waandishi wa habari, ambao pamoja na mambo mengine watatangaza mgeni rasmi wa sherehe hizo pamoja na burudani mbalimbali kwenye mgahawa wa City Sports Lounge.