TFF YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA KIM POULSEN


RAIS wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Leodger  Tenga amemwagia sifa kocha wa sasa wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mdenmark Kim Poulsen kwamba ni mtu wa kazi na hajui anasa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana katika ofisi za TFF jijini Dar es Salaam, Tenga alisema kuwa kwa mwenendo huo, anamatumaini naye makubwa katika kukiletea mafanikio kikosi hicho kwani  akitoka nyumbani kwake amekwenda sokoni au kazini na hajui baa wala sehemu za starehe.
Alisema kwamba matumaini yao kwa Kim ni kutokana na timu yake ya sasa kuundwa na asilimia kubwa ya vijana walio na wastani wa umri wa miaka 23 na kwamba hata wakubwa wachache, rika la akina Juma Kaseja na Haruna Moshi ‘Boban’ wana miaka isiyozidi 27.
Aliongeza kuwa, kwa jitihada alizozionyesha hawana budi kumpongeza Kim na vijana wake kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Gambia, Jumapili katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil na ameomba timu hiyo iungwe mkono zaidi ili ifike mbali.
“Tumefika hapa baada ya jitihada kubwa, ikiwemo kubadilisha kocha. Kupambana na nidhamu, tulimuambia mwalimu, tafadhali, hakikisha nidhamu, utendaji na jitihada za mazoezi, usiogope mchezaji, ita mchezaji, nampongeza sana na hakuna jambo la ajabu kwa sababu tunamjua Kim, ni mtu wa kazi, mwaka mzima”alisema Tenga.
Tenga aliongeza kuwa, tangu kocha huyo awasili  mwaka jana alianzisha programu nzuri ya vijana ambao amekuwa akiwakusanya kila mwezi na kuwanoa jambo ambalo limesababisha hivi sasa awe na timu nzuri ya taifa, baada ya kupandishwa kutoka kocha wa timu za vijana, hadi ya wakubwa, akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
“Wale vijana Sure Boy (Salum Abubakar) na Damayo (Frank) wamecheza pamoja karibu mwaka mzima timu ya vijana chini ya Kim na wanaelewana sana. Sasa tumekwishaanza kuandaa utaratibu wa kuwapatia vijana wataalamu wa saikolojia, ili wawafundishe mambo, namna ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, kuweza kujiami na kadhalika,”alisema
Kama hiyo haitoshi, Tenga alisema wameboresha maslahi ya wachezaji wa Stars ambapo wakishinda wanapata asilimia 15 ya mapato, wakitoa sare asilimia tano, ila wakifungwa hawapati kitu, pia wanampango wa kuwakatia bima.
Taifa Stars hivi sasa inashika nafasi ya pili katika Kundi C, kwa pointi zake tatu, mabao mawili ya kufunga na matatu ya kufungwa, nyuma Ivory Coast inayoongoza kwa pointi zake nne, mabao manne ya kufunga na mawili ya kufungwa, wakati Morocco inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake mbili, mabao matatu ya kufunga na matatu ya kufungwa na Gambia yenye pointi moja, mabao mawili ya kufunga na matatu ya kufungwa inashika mkia.
Stars Jumapili itahamishia mawindo yake katika kinyang’anyiro cha tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini kwa kumenyana na Msumbiji mjini Maputo na inatarajiwa kuondoka nchini Ijumaa. Katika mchezo wa kwanza, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 Dar es Salaam na Stars inatakiwa lazima kushinda ugenini ili kuitoa Mambas na kusonga mbele.