KIM POULSEN AKUNWA NA KIWANGO STARS

LICHA ya kulala mabao 2-0 kwa Ivory Coast ‘The Elephants’ katika mechi ya kwanza ya mchujo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya soka Tanzania, ‘Kilimanjaro Taifa Stars’ Mdenish Kim Poulsen amesema vijana wake walicheza vema na wanaonesha matumaini.
Poulsen alisema, Ivory Coast ni timu bora na bila shaka walikuwa na kikosi chenye uzoefu mkubwa ikilinganishwa na Stars, lakini wachezaji wake walicheza mpira mzuri na wanampa matumaini katika mechi zijazo.
Poulsen, aliyasema hayo jana asubuhi, wakati Stars ambayo kwa sasa inadhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ikiwa mazoezini kujiandaa na mechi dhidi ya Gambia itakayochezwa Dar es Salaam Jumapili ijayo.
“Tunakubali matokeo kwa sababu kikosi chao kina wachezaji wazuri na sisi tunahitaji muda na naamini tutafanya vizuri…nafurahi kuwa wachezaji wameweza kuamka vizuri na kuendelea na mazoezi ili kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Zambia,” alisema Poulsen.
Mechi dhidi ya Ivory Coast, ilichezwa uwanja wa Felix Houphouet Boigny, ambako mabao ya washindi yalipatikana kila kipindi, dakika ya tisa kwa bao la mshambuliaji wao wa kimataifa anayekipiga Chelsea ya England, Solomon Kalou.
Mara baada ya bao hilo, ngome ya Taifa Stars ilitulia na kufanikiwa kutengeneza nafasi mbili za mabao, ambako Mrisho Ngassa na Mbwana Samatta walishindwa kuzitendea haki.
Dakika ya 12, Aggrey Morris alimkwatua mshambuliaji mahiri, Didier Drogba na kulimwa kadi ya njano, kabla ya dakika ya 17, Morris akiwa nje ya kumi na nane katika lango la Ivory Coast, alipiga shuti kali na mpira kugonga mwamba na kuokolewa na mlinda mlango wa Ivory Coast, Barry Boubacar.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Ivory Coast walikuwa mbele kwa bao hilo huku kipindi cha pili kikianza kwa washambuliajiGervinho na Didier Drogba kukosa mabao.
Katika kipindi hicho, makocha wa timu zote walifanya mabadiliko, ambako kocha Paulsen alimwingiza John Bocco na kumtoa Salum Abubakar, wakati kocha wa Ivory Coast, Sabri Lamouch alimtoa Tiote Ismael na kumwingiza Yakonan Didier, Gervinho akapokelewa na Keita Kader, mabadiliko ambayo yaliisaidia Taifa Stars kidogo na kwa Ivory Coast ikaongeza mashambulizi.
Katika dakika ya 69, Aggrey Morris alipewa kadi ya njano ya pili baada ya kumkwatua mchezaji wa Ivory Coast, Goso Goso hivyo kulimwa kadi nyekundu.
Baada ya Morris kutolewa, ilibidi Poulsen amtoe Bocco na kumwingiza Erasto Nyoni, pia limtoa Amir Maftah na kumwingiza Omary Salum, lakini alikuwa Drogba aliyepigilia bao la pili.
Wakati kocha wa Ivory Coast, Lamouch akisifia mchezo wa Taifa Stars huku Solomon Kalou na Yaya Tourre ambaye hakucheza, hawakusita kumsifia Mbwana Samatta na wachezaji wengine wa Stars kwa mchezo walioonesha.
Taifa Stars inatarajiwa kuondoka jijini hapa leo usiku kurudi nchini.
CHANZO:GAZETI LA TANZANIA DAIMA

Comments