WANAMUZIKI WAITWA KUREKODI KAZI STUDIO MPYA ZA MAKUMBUSHO YA TAIFA

Mhandisi wa sauti katika studio za makumbusho Sixmund Begashe akiwaeleza waandishi wa habari mambo mbalimbali kuhusiana na studio hiyo ya Makumbusho ya Taifa

WANAMUZIKI nchini wametakiwa kwenda kurekodia nyimbo zao za mahadhi tofauti na kwa gharama nafuu kwenye studio ya kisasa inayomilikiwa na Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Makumbusho hayo Dk. Paul Msemwa, aliwaambia waandishi wa habari leo lengo la studio hizo ni kusaidia wasanii na hasa wale wanaochipukia.
Ziara ya waandishi hao ni katika  kuelekea kwenye kilele cha siku ya Makumbusho Duniani inayoadhimishwa kesho.
Dk. Msemwa alisema studio hiyo ilizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka jana kwa lengo la kuwasaidia wanamuziki wa kiasili zaidi na wanaochipukia, ambapo ina vifaa vya kisasa zaidi kuliko zote Afrika Mashariki.
“Gharama za kurekodi kwenye studio yetu zipo chini ukilinganisha na studio nyingine, hii ni kwa sababu tumelenga kuwasaidia wanamuziki wachanga hasa wanaopiga midundo yenye vionjo vya kiafrika zaidi,” alisisitiza mkurugenzi huyo.
Awali alibainisha kuwa tangu kufunguliwa kwa studio hiyo wiki kadhaa zilizopita, hakuna mwanamuziki aliyefanya kazi hapo kwa sababu hawafahamu kwamba imeanza kazi ama la.
“Hii ni studio mpya hivyo wengi hawajui kama tumeanza kazi, ukweli ni kwamba hii ni studio ya kisasa zaidi kwa maana ya vifaa vyake kuliko studio nyingine Afrika Mashariki,” alisisitiza Dk. Msemwa ambaye ni Mtaalam wa Uhifadhi na Mambo ya Kale.
Katika kuadhimisha siku ya makumbusho duniani, uongozi wa Makumbusho hapa nchini umewataka Watanzania kote nchini kutembelea makumbusho zilizopo kwenye maeneo yao, ambapo watoto wasiozidi miaka 16 na wazee wanaozidi miaka 65 wataingia bure huku wengine wakiingia kwa sh 1,500.

Comments