WANACHAMA 700 WAMNG'OA NCHUNGA YANGA

WANACHAMA wapatao 700 wa klabu ya Yanga, jana kwa kauli moja walitangaza kuung’oa madarakani uongozi wa Lloyd Nchunga katika mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaunda, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulioratibiwa na Baraza la Wazee kwa kushirikiana na vijana, ulihamia kwenye uwanja huo kutokana na idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kuamua hatima ya klabu yao.
Katika mkutano huo uliodumu kwa saa mbili, kuanzia majira ya saa 6 hadi 8 mchana, muda ulivyokuwa ukisogea, ndivyo wanachama walivyokuwa wanaongezeka.
Ingawa mkutano huo ulianza na wanachama wapatao 556, lakini hadi unafungwa, walikuwa wamefikia 700, wote kwa pamoja wakiridhia kuuweka kando uongozi wa Nchunga.
Baada ya mkutano huo kufunguliwa na dua na sala, Katibu wa Wazee, Ibrahim Akilimali, alitoa maneno machache kuelezea udhaifu wa uongozi wa Nchunga tangu uingie madarakani Julai 18, 2010.
Akilimali aliwaeleza wanachama kuwa, kutokana na mambo kutokwenda sawa katika klabu yao, ndiyo maana waliamua kuchukua jukumu la kuitwaa timu kuelekea mechi ya Simba.
Alisema, sababu ya wao kufikia hatua hiyo, ni wachezaji kukosa ari ya kucheza kutokana na matatizo ya uongozi wa Nchunga ikiwemo kutolipwa mishahara, hivyo kuishi kwa dhiki kubwa.
“Ndugu zangu, tulitaka tuchukue timu kwa nia ya kuepuka kufungwa na Simba, awali Nchunga aliridhia, lakini baadaye aligeuka, nasi tukajiweka kando na matokeo yake umeyaona (Yanga ilichapwa mabao 5-0),” alisema Akilimali akishangiliwa na wanachama wenzake.
Alisema hatua ya kumtaka Nchunga akae kando, ni kutokana na kushindwa kuongoza kwani kuna hatari ya klabu hiyo kuingia kwenye madeni yatakayogharimu uhai wake.
Akilimali alisema, udhaifu na matatizo ya uongozi wa Nchunga, yanathibitishwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioamua kumsusia klabu hiyo. 
Alisema, miezi michache tangu kuingia madarakani, makamu wake, Davis Mosha alijiuzulu akifuatiwa na wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji hivi karibuni, hivyo hafai kubaki Yanga.
Mbali ya Mosha, wengine walioachia ngazi, ni Seif Ahmed, Ally Mayay, Edgar Chibula na Abdallah Bin Kleb, ambao wote walifanya hivyo kutokana na matatizo yaliyomo kwenye uongozi wa Nchunga.
Kuhusu fedha za kuendesha timu, Akilimali alisema tayari wameahidiwa kupewa sh mil 750 na watu wenye mapenzi na klabu hiyo, na kwamba kuna mfanyabiashara mmoja ameahidi kutoa sh mil 250, hivyo kufikia sh bil 1.
Kati ya waliopewa nafasi ya kusema machache, ni kipa wa zamani wa timu hiyo, Hamisi Kinye na beki Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, ambao waliushutumu uongozi wa Nchunga kwa usajili mbovu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, iwapo theluthi ya wanachama watajiorodhesha na kutia saini zao, maamuzi watakayofikia, ni halali.
Baada ya kupitisha uamuzi huo, Akilimali alisema watawasilisha orodha ya wanachama waliojiorodhesha kushiriki mkutano huo kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo Wilaya ya Ilala kuomba uchaguzi mkuu.
Tangu Yanga ipoteze mwelekeo wa ubingwa wa Ligi Kuu, kumekuwa na harakati za kuung’oa uongozi wa Nchunga kwa hoja ya kushindwa kazi, huku wachezaji na makocha wakilia kutolipwa mishahara.

Comments