MSANII wa filamu nchini ambaye pia huiga sauti za viongozi
mbalimbali, Steve Mengele 'Steve Nyerere' jana amezindua filam yake mpya inayojulikana kama
'Mwalim Nyerere'.
Filam hiyo ameizindua kwa staili tofauti ambapo badala ya
kuzindua Ukumbini kama ilivyozoeleka na wengi,
msanii huyo amezindua filam hiyo katika kituo cha watoto yatima cha Maunga
Centre kwa kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 3
ikiwa ni pamoja na kujitolea kuwasomesha watoto wawili katika kituo hicho.
Akizungumza mara baada ya kuzindua filamu hiyo akiwa pamoja
na watoto yatima wa kituo hicho, Steve Nyerere alisema ameamua kufanya hivyo
kutokana na ukweli kwamba Baba wa Taifa Mwali Nyerere hakubagua watu.
Alisema ujio wa filamu hiyo ni kama
azma yake aliyoipanga tangu awali kuhakikisha anamuenzi Baba wa Taifa kwa kutoa
filamu itakayokuwa inaonesha mambo mbalimbali aliyowahi kuyafanya Baba wa
Taifa.
"Jina lililonibeba zaidi katika tasnia hii ya filamu ni
jina la Steve Nyerere kiasi ambacho hata jina la Baba yangu halijanizoea, hivyo
kutokana na ukubwa wa jina hili limenifanya mimi kutambulika na jamii nzima ya Tanzania hivyo
ili kulienzi jina hili nimeamua kutoa filamu hii ya Mwalim
Nyerere,"alisema Steve.
Alisema msaada alioutoa kwa watoto yatima hautaishia kwao
bali ataendelea kutoa kile atakachokipata kupitia filamu hiyo kuwasaidia na
wale wasiojiweza.
Alisema filam ya Mwalim Nyerere ameifanyia Butiama
alipozaliwa Baba wa Taifa ili kujenga uhalisia wa kile alichodhamiria na kwamba
ameitengeneza filamu hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu huku akishirikiana vema
na mke wa Hayati Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere.
Alisema jumla ya sh. milioni 25 ametumia katika kuikamilisha
filam hiyo ambayo itaanza kuingia sokoni leo ikiwa chini ya usambazaji wa Steps
Entertaiment.
Kabla ya kutoa filam hiyo Steve Nyerere alitamba na filam ya
'Mr President' aliyoitunga kwa kuvaa uhusika wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
Tanzania Dkt.Jakaya Kikwete ambayo aliitaja kama zawadi kwa Rais Kikwete katika
kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.
Comments
Post a Comment