STAMINA TATIZO LA WACHEZAJI TANZANIA-POILSEN



WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, kikitarajia kuondoka alfajiri ya kesho kwenda Ivory Coast kwa mechi ya kimataifa, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen, amesema stamina ni tatizo kubwa kwa nyota wengi.
Poulsen aliyetwaa jukumu hilo hivi karibuni kutoka kwa Jan Poulsen, aliyasema hayo jana wakati akitoa tathmini fupi juu ya mazingira ya kikosi chake tangu akabidhiwe jukumu hilo wiki mbili zilizopita.
Alisema, pamoja na wachezaji wengi kuwa na uwezo mkubwa kiuchezaji, suala la stamina limekuwa tatizo kwa wachezaji wengi, hivyo kushindwa kucheza kwa kasi na ufanisi kwa dakika zote 90.
Alisema kutokana na dosari hiyo, tayari ameanza kuchukua hatua kwa kufanya mazungumza na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuangalia njia bora ya kuondoa tatizo hilo kwa kushirikiana na makocha wa timu nyingine.
“Kwa upande wa Stars, nimeshaanza nalo kwa kuwapa  mazoezi ya ziada baada ya mazoezi ya kawaida. Kwa kweli, wachezaji wameonekana kuyakubali,  wameridhishwa nayo na kuyafurahia, binafsi inanitia moyo,” alisema.
Kim alisema mbali ya stamina, pia amekuwa akiwasihi wachezaji wake kuwa na moyo wa kujituma, akisema hicho ni kitu muhimu kwa timu katika kupigania ushindi na mafanikio ya timu.
Aidha, Poulsen alisema ndani ya kipindi cha wiki mbili alizodumu na timu hiyo, wachezaji wameanza kuelewa falsafa yake, hivyo kumpa matumaini ya kuwa na kikosi bora zaidi katika siku za usoni.
Hata hivyo, ameishauri TFF kuwa, wachezaji wote ambao watakuwepo kambini kipindi cha maandalizi ya mechi, wote wawe wanasafiri na timu (hata kama hawatacheza), kwa lengo la kuwapa nafasi ya kujifunza zaidi.
Katika hatua nyingine, Kim amekana kufanya upendeleo katika uteuzi wa kikosi cha kwanza, hasa katika mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi, akisema alichagua kutokana na uwezo na sifa zao.
Aliongeza kuwa, nyota wake Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu  watabaki kutokana na kuwa majeruhi waliyopata wakati wa mazoezi yao, hivyo watabaki kujinoa kabla ya kuungana na wenzao watakaporudi kujiandaa dhidi ya Gambia.
Nyota wa Stars ni makipa: Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally (Azam) na Deogratius Munishi (Mtibwa Sugar). Mabeki: Nassor Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Simba), Waziri Salum (Azam), Shomari Kapombe (Simba) na Juma Nyoso (Simba).
Viungo ni Mwinyi Kazimoto (Simba), Salum Abubakar (Azam), Jonas Mkude (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Edward Christopher (Simba - U20), Mrisho Ngasa (Azam) na Frank Domayo (JKT Ruvu- U20).
Washambuliaji ni Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Ramadhan Singano (Simba -U20), Simon Msuva (Moro United - U20),  Haruna Moshi (Simba) na John Bocco (Azam). 

Comments