SIMBA YAMTIA PINGU MILOVAN

Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage kulia, Milovan katikati na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Ibrahim Masoud walipokuwa wakisaini mkataba wa kwanza na Mserbia huyo mwaka jana.
KLABU ya Simba ya Dar es Salaam imemuongezea mkataba wa miaka miwili kocha wake Mserbia, Profesa Milovan Cirkovic baada ya kuridhishwa na kazi yake kwa kipindi cha nusu msimu alichokuwa na timu hiyo tangu arithi mikoba ya Mganda, Moses Basena.
Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema jioni hii kwamba Milovan atakuwa kocha wa Simba kwa miaka miwili zaidi tangu sasa baada ya kuongezewa mkataba.
“Kipimo cha mafanikio ya kocha ni mataji na soka safi, kitu ambacho sisi kama viongozi tumekishuhudia Simba chini ya Profesa Milovan, sasa hatuoni kwa nini tusimuongeze mkataba,”alisema Kaburu.
Pamoja na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara kwa kishindo, Milovan aliiwezesha Simba kufika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa kwa penalti 9-8 na Al Ahly Shandy ya Sudan, baada ya sare ya jumla ya 3-3.

Comments