SIMBA WATUA SALAMA SUDAN

Na Ezekiel Kamwaga, Khartoum TIMU ya soka ya Simba imewasili salama jijini Khartoum, Sudan, jana usiku majira ya saa 5;49 ikitokea jijini Nairobi, nchini Kenya tayari kwa pambano lake la Kombe la Shirikisho (CAF) dhidi ya Al Ahly Shendi ya hapa. Simba ilitakiwa kuingia Sudan saa mbili usiku lakini ilichelewa kufika kutokana na hitilafu iliyokuwapo katika ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) iliyopaswa iichukue kutoka Nairobi. Msafara huo wa Simba wa wachezaji 19 na viongozi wanane umefikia katika Hoteli ya Shariqa lakini leo timu itasafirishwa kwenda katika mji wa Shendi uliopo umbali wa Kilomita 150 kutoka Khartoum. Mechi ya Shendi na Simba itapigwa Jumapili hii saa mbili usiku katika Uwanja wa Shendi wenye uwezo wa kuchukua washabiki 10,000. Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum, Simba ililakiwa na uongozi wa Chama cha Soka cha Sudan (SFA) lakini iliwekwa uwanjani hapo kuanzia saa sita usiku hadi saa saba na nusu usiku kwa kisingizio cha kumalizia taratibu za kiulinzi na kiusalama uwanjani hapo. Kiongozi huyo wa SFA alipoulizwa kwanini wachezaji wanazidi kuwekwa uwanjani hapo ilhali usiku wa manane umeingia, kiongozi huyo alijibu tu kuwa “ Hata kwenu pia mlifanya hivihivi.” Hata hivyo Simba iliipokea vizuri Shendi ilipokuja nchini na pia timu hiyo ya Sudan haikufika Dar usiku wa manane bali asubuhi. Kocha Mkuu wa Simba, Profesa Milovan Cirkovic amesema leo asubuhi hatakifanyisha kikosi chake mazoezi ya aina yoyote isipokuwa jioni tu ndipo kitafanya mazoezi. Kuna uwezekano mkubwa wa mazoezi ya leo kufanyika usiku, muda ambao timu hizi mbili zitacheza. Timu zote mbili, Simba na Shendi zinaweza kucheza kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la CAF. Simba iliweza kufika fainali ya michuano hii mwaka 1992 lakini wakati huo mfumo wa sasa wa hatua ya makundi katika hatua ya nane bora ulikuwa haujaanza kutumika. Wachezaji wa Simba waliopo Sudan ni Juma Kaseja, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Derick Walulya, Amir Maftah, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Victor Costa na Obadia Mungusa. Wengine ni Mutesa Patrick Mafisango, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi, Machaku Salum, Uhuru Selemani, Jonas Mkude na Edward Christopher. Wengine katika msafara huo ni Emmanuel Okwi, Felix Sunzu na Gervais Kago. Benchi la ufundi linaongozwa na Milovan, Amatre Richard, James Kisaka, Dk. Cosmas Kapinga na Nicholaus Nyagawa. Viongozi wa Simba waliofutana na timu hiyo ni Mwenyekiti, Mhe; Ismail Aden Rage, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Swedy Mkwabi na Msemaji wa timu, Ezekiel Peter Kamwaga. Mkuu wa ,msafara huo ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Hussein Mwamba.

Comments