SIMBA SC WATESWAJE SUDAN

Na Ezekiel Kamwaga, Khartoum *Walishwa lunch saa 10 jioni *Chakula cha usiku saa sita usiku *Rage, Kisaka, wanyimwa pa kulala, walala mapokezi * Wachezaji wajifua kivyao UONGOZI wa Simba SC unakusudia kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na unyama inaofanyiwa nchini Sudan inakosubiri pambano lake dhidi ya Al Ahly Shendi kesho. Tangu iwasili nchini Sudan juzi, Simba imekuwa ikifanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana na wenyeji wake, Shirikisho la Soka Sudan (SAF) na Al Ahly Shendi. Jana, Simba ilifanyiwa vitendo hivyo kabla ya kwenda katika mji wa Shendi itakakochezwa mechi hiyo na baada ya kufika katika mji huo uliopo takribani kilomita 170 kutoka mji mkuu Khartoum. Simba iliwasili Shendi majira ya saa mbili usiku kwa saa za Sudan (sawa na saa za huko) baada ya safari ya takribani masaa manne kutoka Khartoum. Safari ya kutoka Khartoum hadi Shendi ilianza majira ya saa kumi jioni na timu ikafika saa mbili usiku, kwa maana ya masaa manne ya safari ya barabara jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za CAF zinazozungumzia umbali usiozidi masaa mawili. Ingawa kanuni ya CAF kifungu cha 5 (3) kinazungumzia umbali wa kusafiri kwa basi usizidi kilomita 200, Simba inaweza kutuma malalamiko kwamba kutoka Khartoum hadi Shendi ni zaidi ya kilomita 150 kwa vile si haiwezekani kutumia masaa manne kwa umbali huo. Zaidi ya usumbufu huo wa kusafiri muda mrefu, Simba pia inajiandaa kutuma malalamiko CAF kwa vile hoteli waliyopangiwa haina kiwango kinachokubalika na shirikisho hilo. Kwa mujibu wa kanuni ya CAF kifungu cha 7 (c), timu mwenyeji inatakiwa kuhakikisha kuwa timu mgeni inaishi katika hoteli ya daraja la kwanza na pia msafara mzima unakaa katika hoteli moja. Hata hivyo, Simba imewekwa katika hosteli inayofanana na mabweni ya wanafunzi na imepewa vitanda 24 tu huku msafara ukiwa na watu takribani 30. Wakati ilipokuja Tanzania, Simba ililipia gharama za watu 30 wa timu hiyo na kulikuwa na makubaliano kwamba na wao watafanya hivyo wakati Wekundu watakapokwenda Sudan. Kutokana na ukosefu huo wa vyumba, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alilala kwenye makochi ya chumba cha mapokezi pamoja na kocha msaidizi wa makipa wa Simba, James Stephan Kisaka. Viongozi wengine wa Simba, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Swedy Mkwabi na kiongozi wa msafara, Hussein Mwamba ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, pia walikosa pa kulala na hivyo wakalazimika kwenda kulala nje ya hosteli hiyo ya Shendi. Wakizungumzia hali hiyo, wawakilishi wa timu ya Shendi walidai kwamba inatokana na ukweli kuwa mji wao ni mdogo na hakuna hoteli nyingine kubwa kuliko hiyo mji mzima. “Kusema kweli mlitupokea vizuri sana tulipokuja Dar es Salaam na hatuna malalamiko yoyote yale. Hata hivyo, huu ndiyo uwezo wetu na hatuna la kufanya. Hata Ferroviaro ya Msumbiji walikaa hapahapa walipokuja hapa, alisema Hamdy Ibn Hossein,” mwakilishi wa Shendi. Rage alisema Simba itacheza mechi yake dhidi ya Shendi wakati tayari ikiwa imewasilisha malalamiko yake CAF kupitia kwa kamisaa wa pambano hilo ambaye alitarajiwa kuwasili hapa jana jioni (Ijumaa). “Hawawezi kusema kwamba kwa sababu Ferroviarro walikaa hapa basi na sasa tukae. Hii si hoteli inayosemwa na CAF, hii ni hosteli ya kuweka wanafunzi. Huu ni uvunjaji wa wazi wa kanuni na tunaukataa,” alisema. Ingawa Simba iliwasili Shendi saa mbili usiku, chakula kilicheleweshwa hadi saa sita usiku ambako wachezaji waliamshwa kula jambo linaloonyesha kuwa hujuma zimepangwa. Jana, magazeti ya Tanzania yaliripoti kuhusu Simba ilivyotelekezwa katika hoteli ya Safiga jijini Khartoum kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi jioni bila ya taarifa yoyote huku wenyeji wakidai wamekwama kwenye foleni. Kutokana na Simba kuingia Shendi usiku, Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic, aliamua kuwapa wachezaji mapumziko hadi jana lakini wachezaji waliamua kujifanyia mazoezi wenyewe. Mmoja wa wachezaji waliokuwa wakijifanyia mazoezi binafsi ambayo yanajulikana kwa jina la individual, alikuwa ni Haruna Moshi Boban ambaye alikutwa akifanya mazoezi ya peke yake kuzunguka eneo la hosteli ilikofikia timu. “Tangu juzi hatujafanya mazoezi kwa sababu ya safari na vituko vya hawa wenyeji wetu. Nimeamua kujifua mwenyewe kwa sababu ukikaa muda mrefu bila mazoezi hata mwili nao unazoea ulegevu. Ndiyo maana najifua,” alisema. Zaidi ya Boban, wachezaji wengine waliokutwa wakifanya mazoezi majira hayo ya saa tano usiku ni Mwinyi Kazimoto, Juma Kaseja, Patrick Mafisango, Shomari Kapombe, Uhuru Selemani na Emmanuel Okwi. Katika mechi ya kwanza iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 na inahitaji sare ya aina yoyote au kufungwa chini ya mabao 3-0 ili kusonga mbele.

Comments

  1. Simba wapambane kiume tu, mafanikio hazaji kirahisi hizo hujuma zinatokana na hao jamaa kutambua ubora wa simba ila wao wasitetereke japo inabidi simba wajiandae kwa hujuma nyingine ndani ya uwanja na wasipokuwa makini yatatokea yale ya Algeria kadi nyekundu mwanzoni kabisa mwa mchezo.
    Kila la kheri simba

    ReplyDelete

Post a Comment