PRISONS:HATUTARUDIA MAKOSA

BAADA ya kufanikiwa kurejea Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, timu ya maafande wa Tanzania Prisons ya Mbeya, imeapa kutorudia makosa yaliyoifanya ishuke daraja misimu miwili iliyopita na tayari imeanza kujipanga kwa msimu ujao wa Ligi. Msemaji wa idara ya michezo wa Jeshi la Magereza Tanzania, Mrakibu Mwandamizi (SSP), Elisha Kitojo, alisema kuwa, wamejifunza kwamba, wanapaswa kufanya kila wawezalo kuhakikisha hawashuki daraja, kwa vile Ligi Daraja la Kwanza ni ngumu mno. Alisema, ili timu iweze kufanya vema katika Ligi daraja la kwanza, inapaswa kujipanga kutokana na timu kuwa nyingi na inapofikia hatua ya tisa bora, kuna vikwazo vinavyotokana na mambo kadhaa, lakini tatizo likiwa kwa timu mwenyeji kuwa na nafasi kubwa ya kupanda. “Tanzania Prisons tunashukuru kwamba tumefanikiwa kurejea Ligi Kuu hivi sasa, hatutakubali tena kushuka daraja kwa kuwa huko ni kugumu na hakufai, ili kuhakikisha hayo hayatukuti tena, tunasubiri ripoti ya mwenyekiti wa timu yetu ili tuanze kujipanga,” alisema Kitojo. Alisema kuwa, wanasubiri kuipitia ripoti hiyo, ambayo ilitarajiwa kuwafikia jana, hivyo wanaweza kuanza kuipitia kuanzia leo na baada ya hapo wataanza kujipanga kwa ajili ya msimu ujao, ikiwa ni pamoja na kufanya usajili na kisha kuanza mapema maandalizi ya Ligi kuu.

Comments