PAMOJA NA KUJIUZULU NCHUNGA AENDELEA KUKABWA KOO


Baraza la Wazee la klabu ya Yanga, limepongeza uamuzi wa Nchunga kujiuzulu na kuwa, baada ya zoezi hilo wanasubiri mwongozo toka TFF ili waweze kuendelea na mchakato mwingine, ukiwemo wa kukabidhi timu kwa baraza la wadhamini ambalo litasimamia usajili wa wachezaji na mambo mengine.
Hata hivyo, baraza hilo kupitia kwa Katibu wake, Ibrahim Akilimali, walisema kwamba, kujiuzulu kwa Nchunga kunamaanisha kuwa, hata wajumbe wengine waliogoma kuachia ngazi kama walivyowataka, nao hawawatambui kama ni viongozi wa Yanga.
Aliongeza kuwa, pamoja na kuziuzulu huko, bado wanaendelea na mpango wao wa kufika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU), pamoja na wizara yenye dhamana na michezo, ili kukagua mali za Yanga, kwani wanaamini kulikuwa na ubadhirifu mkubwa.
Juzi, Nchunga alitangaza kujiuzulu wadhifa wake huo kufuatia msigano baina yake na baadhi ya wanachama wa Yanga wakiongozwa na Baraza la Wazee, kumtaka ajiweke kando kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio klabu hiyo, ambayo ilijikuta ikipokwa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliokwenda kwa mahasimu wao Simba.

Comments