NYOSO,UHURU SELEMAN WAITESA YANGA


 KLABU ya Yanga imeanza mkakati wa kuwasajili wachezaji kadhaa kutoka kwa watani wao Simba, wakiwamo mabeki Juma Jabu, Juma Nyoso na kiungo Uhuru Suleiman.
Kwa mujibu wa habari zilizoifikia Tanzania Daima na kuthibitishwa na mmoja wa viongozi wa klabu hiyo anayehusika na usajili, wameamua kuwafukuzia nyota hao kutokana na mikataba yao Simba kukaribia mwishoni.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa, kwa sasa wapo kwenye mazungumzo ya awali na nyota hao, ingawa bado hawajafikia hatua ya mwisho kwa ajili ya kusaini fomu za usajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu.  

Yanga imekuwa na mkakati wa kusuka kikosi cha ushindi baada ya kushindwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu iliyofikia tamati Mei 6, ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam FC.
Kama unavyojua, Yanga imekuwa mbovu katika siku za hivi karibuni na matokeo yake tulipoteza ubingwa wa  Ligi Kuu Bara na nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao, sasa hatutaki kurudia makosa, tunataka kufanya usajili mzuri kurejesha heshima yetu,” alisema kiongozi huyo.
Aliongeza, mbali ya hao,  pia wana mpango wa kuimarisha safu ya ushambuliaji kwa kusajili wawili kutoka nchini Rwanda ambao ni Meddie Kegere na Olivier Karekezi, waliong’ara kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, lililofanyika Desemba, 2011, jijini Dar es Salaam.
Chini ya ufadhili wa Yusuf Manji aliyerejea kuokoa jahazi, Yanga wamepania kusajili nyota mahiri na kuajiri kocha bora atakayeziba nafasi ya Mserbia, Kostadin Papic, aliyemaliza mkataba wake mapema mwezi huu.

Comments