NURDIN, ULIMWENGU WAPELEKA AHUENI STARS

KIM Poulsen, kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), amesema kupata nafuu na kurejea uwanjani kwa kiungo, Nurdin Bakari ni suluhisho la udhaifu katika safu ya kiungo ya timu hiyo. Bakari na mshambuliaji, Thomas Ulimwengu jana waliungana na wenzao katika mazoezi ya asubuhi kwenye Uwanja wa Karume ikiwa ni baada ya kuwa nje kwa zaidi ya wiki moja kutokana na kuwa majeruhi.

Ulimwengu alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, wakati Bakari alikuwa majeruhi wa kifundo cha mguu.

Akizungumza mara baada ya mazoezi, Kim alisema endapo Bakari atapona haraka, basi atakuwa kwenye mpango wake wa kumtumia kwa ajili mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Ivory Coast baadaye mwezi ujao.

"Kama nilivyosema awali, kwa sasa nashughulikia kutafuta ufumbuzi wa matatizo niliyoona kwenye mechi dhidi ya Malawi kabla ya kuivaa Ivory Coast. Nachofurahi ni kurejea mazoezini kwa Bakari na Ulimwengu. Hawa ni wachezaji muhimu wanaweza kutusaidia kwenye mechi inayofuata. Bakari ni mzoefu mkubwa wa sehemu ya kiungo," alisema Kim.

Kim ambaye amekuwa akikosoa ubinafsi na kusisitiza umuhimu wa wachezaji wa kucheza kitimu, aliwakingia kifua chipukizi wake kwa kusema bado wanahitaji muda ili waweze kupata uzoefu.

"Uzoefu ni muhimu kwenye kazi yoyote ingawa hata yule asiyenao anatakiwa apewe fursa ili na yeye apate. Frank Domayo hakucheza vibaya siku ila alikosa uzoefu, Nurdin Bakari ni mzoefu anaweza kusaidia." Kim.

Aidha, Kim amewataka wachezaji wake kutohofia majina makubwa ya wachezaji wa Ivory Coast siku watakapopambana nao ugenini mjini Abidjan.

Ivory Coast ina wachezaji wenye majina makubwa kama Didier Drogba, Yahya Toure, Kolo Toure and Solomon Kalou wanaocheza soka Ligi Kuu England.

Alisema ana imani wachezaji wake wana sifa ya kimataifa na amewataka kutokuwa na hofu ya majina, bali wacheze kwa kushambulia kwa vile ni muhimu kupata bao ugenini.

CHANZO:GAZETI LA MWANANCHI

Comments