MZEE SMALL AUGUA GHAFLA,ALAZWA AMANA


MWIGIZAJI mkongwe wa vichekesho nchini, Saidi Ngamba, maarufu kwa jina la Mzee Small, amelazwa katika Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam, baada ya kuugua ghafla.
Mzee Small anayesumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu kiasi cha kushindwa kuongea; aliugua ghafla juzi jioni muda mfupi baada ya kutoka Mwanza alikokwenda kwenye shughuli za kisanii.
Mwigizaji mwenzake Chausiku Salum Maele ‘Bi Chau,’ alisema kabla ya kuugua, Mzee Small alikuwa mwenye afya njema, hadi walipoachana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) walikirejea kutoka Mwanza.
Kwa mujibu wa Bi. Chau, walikwenda Mwanza Ijumaa iliyopita kusherehesha shughuli ya walemavu wa ngozi ‘Albino,’ iliyoandaliwa na madaktari wa Hospitali ya Bugando, jijini humo.
“Tuliondoka Dar es Salaam na ndege ya jioni Ijumaa tukalala Mwanza, Jumamosi tukafanya kazi iliyotupeleka. Jumapili jioni tuliondoka Mwanza kuja Dar, sasa kabla sijafika nyumbani kwangu Magomeni nikapokea simu kutoka kwa binti yake Small, akanipa taarifa za ugonjwa, nilishtuka,” aliongeza Bi Chau swahiba wa nguli huyo wa vichekesho.
Tanzania Daima ikampigia mke wa Mzee Small, ambapo alisema bado hali ya mumewe haijatengemaa hivyo kuomba dua za Watanzania.
“Ana tatizo la presha na huwa anajikuna na kuvimba, lakini safari hii amevimba shavu moja na kadiri muda unavyokwenda hali yake inazidi kuwa mbaya,” alisema mke huyo akiwa nyumbani kwake Tabata Kimanga kabla ya kumpeleka hospitali.
Katika maelezo ya mke huyo wa Mzee Small, alisema juzi usiku walimpeleka mumewe Hospitali ya KLM iliyoko Tabata, ambapo alipewa dawa ya kupunguza shinikizo la damu kisha kuruhusiwa kurudi nyumbani na kwamba hali ya msanii huyo iliendelea kuwa mbaya hadi alipokimbizwa Hospitalli ya Amana jana mchana.
CHANZO:GAZETI LA TANZANIA DAIMA

Comments

Post a Comment