MTWARA, KIGOMA, MARA WENYEJI LIGI YA TAIFA

Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepanga vituo vitatu vya Ligi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa kwa ajili ya ligi hiyo itakayoanza Mei 26 mwaka huu. Kundi A lenye mabingwa wa mikoa ya Iringa (Kurugenzi Mufindi), Lindi (Lindi SC), Mbeya (Tenende FC), Morogoro (Mkamba Rangers), Mtwara (Ndanda SC), Pwani (Super Star), Rukwa (Mpanda Stars) na Ruvuma (Mighty Elephant) zitacheza mechi zake mjini Mtwara. Mji wa Kigoma utakuwa mwenyeji wa mabingwa wa mikoa ya Dodoma (CDA), Kagera (Bandari FC), Kigoma (JKT Kanembwa), Mwanza (Pamba SC), Shinyanga (Mwadui SC), Singida (Aston Villa) na Tabora (Majimaji). Kundi C lenye mabingwa wa mikoa ya Arusha (Flamingo SC), Dar es Salaam (Ashanti United ya Ilala, Red Coast ya Kinondoni na Tessema FC ya Temeke), Kilimanjaro (Forest FC), Manyara (Nangwa VTC), Mara (Polisi Mara) na Tanga (Korogwe United) watachezea mechi zao mkoani Mara. Mwisho wa kuwasilisha fomu za usajili ni Mei 15 mwaka huu wakati kipindi cha pingamizi ni kuanzia Mei 16 hadi 22 mwaka huu. Mei 23 mwaka huu Kamati ya Mashindano ya TFF itakutana kupitia usajili huo. Wachezaji wanaosajiliwa ni wale wale waliochezea timu hizo katika ligi ya mkoa. Mei 14 mwaka huu ni mwisho kwa mikoa yenye pingamizi kwa mabingwa wao kuwa wameshashughulikia rufani husika. Kamati ya Mashindano imeagiza kuwa kwa mikoa itakayoshindwa kufanya hivyo mpaka baada ya tarehe hiyo mabingwa wao hawatashiriki ligi hiyo. Timu tano zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao. Mshindi wa kwanza kutoka kila kundi na washindwa wawili bora (best losers) kutoka kundi A na C ambayo yana timu nane kila moja.

Comments