MASHAUZI CLASSIC, MASHUJAA MUSICA KUPAMBA MISS TABATA 2012


Na Mwandishi Wetu
BENDI za Mashujaa na Mashauzi Classic zitatumbuiza kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mrembo wa Tabata, Miss Tabata 2012 kitakachofanyika Juni Mosi katika ukumbi wa Da West Park, Tabata.
Akizungumza jana, mratibu wa shindano hilo, Godfrey Kalinga, alisema kuwa wameamua kuweka burudani nyingi yenye ladha tofauti ili kukidhi kiu ya rika zote watakaohudhuria shindano hilo ambalo ni kivutio kwa wakazi jijini.
Kalinga alisema shindano hilo pia litatumika kwa ajili ya kusherehekea miaka 10 tangu kuasisiwa kwa shindano la Miss Tabata.
“Shindano la mwaka huu litakuwa ni la aina yake kwa sababu hii utakuwa ni mwaka wetu wa 10 tangua kuanza kuandaa Miss Tabata ndio maana tunaleta burudani nyingi,” alisema mratibu huyo wa Bob Entertainment na Keen Arts.
Alisema warembo waliyowahi kushinda mataji mbalimbali ya shindano hilo, pia wamealikwa kusherehekea miaka 10 ya Miss Tabata.
Shindano hili limedhaminiwa na Dodoma Wine, Redds, Integrated Communications, Fredito Entertainment, Multichoice Tanzania, Screen Masters, Kitwe General Traders, Step In Electronics, Brake Point, Atriums Hotel na Lady Pepeta.
Warembo watakaoshiriki kwenye shindano wanaendelea na mazoezi kila siku katika ukumbi wa Dar West Park.
Warembo hao ni Neema Saleh (18), Noella Michael (19), Queen Issa (20), Hycalisa Joseph (18), Phillios Lemi (19), Wikllihemina Mvungi (20) na Nightness Rajab (19).
Wengine ni Suzanne Pancras (19), Caroline David (21), Khadija Nurdin (19), Jamila Omary (18), Advent Mamkwe (21), Nadya Marjeby (21), Axer Peter (20), Rahama Hassan (19), Mercy Mlay (21) na Diana Simon Laizer (20).
Warembo 10 watachaguliwa kushiriki mashindano ya Miss Ilala na baadaye Miss Tanzania.
Mrembo anayeshikilia taji la Tabata kwa sasa ni Faiza Ally.
Warembo wa Tabata wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya Miss Tanzania ambapo mwaka juzi Consolata Lukosi alishinda nafasi ya tatu kabla ya kutangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Redds.
Katika shindano la mwaka juzi Juliet William pia alishinda nafasi ya tatu katika ngazi hiyo ya taifa.
Juliet ndiye anayeshikilia taji la dunia la Miss Progressive International.

Comments