Timu za Taifa za Tanzania
(Taifa Stars) na Malawi (The
Flames) zinapambana kesho (Mei 26 mwaka huu) katika mechi ya kirafiki
itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Makocha wa timu zote mbili, Kim Poulsen wa Taifa Stars na
Kinnah Phiri wa The Flames wamezungumzia umuhimu wa mechi hiyo katika Mkutano
na Waandishi wa Habari uliofanyika leo (Mei 25 mwaka huu) ofisi za Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
Kim ambaye hiyo itakuwa mechi yake ya kwanza tangu asaini
mkataba wa kuinoa Stars, amesema baada ya mazoezi ya siku kumi hicho ndicho
kipimo chake cha kwanza na cha mwisho kabla ya kucheza na Ivory Coast kwenye
mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayofanyika ugenini Juni 2 mwaka huu.
“Wachezaji wangu wamekuwa wakipokea mafunzo vizuri ingawa
Nurdin Bakari na Thomas Ulimwengu hatakuwepo kwa vile ni majeruhi. Bila shaka
baada ya mazoezi ni lazima ujipime, hivyo mechi hii ni muhimu kwangu
ukizingatia kuwa kwenye ubora wa viwango vya FIFA, Malawi wako juu yetu,” amesema Kim.
Naye Phiri ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malawi amesema awali aliombwa mechi na Misri,
lakini akaamua kucheza na Taifa Stars kwa vile anaamini kitakuwa kipimo kizuri
kwake kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Kenya itakayofanyika Juni 2 mwaka huu jijini Nairobi .
“Nimekuja na wachezaji 20 ambapo nusu yao
wanacheza mpira wa kulipwa nje ya Malawi ,
wengi wakiwa Afrika Kusini lakini wapo pia kutoka Msumbiji na mmoja anacheza
Hispania katika timu ya vijana ya Atletico Madrid . Tumejianda si kwa mechi hii tu, bali
pia dhidi ya Kenya na
baadaye Nigeria
ambao tutacheza nao numbani Juni 9 mwaka huu,” amesema Phiri ambaye kwenye
benchi lake la ufundi anasaidiwa na Young Chimodzi.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa viti vya
kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B
wakati VIP A inayochukua watazamaji 748 tu itakuwa sh. 20,000.
Comments
Post a Comment