MAKOCHA RIADHA WAPONGEZA UCHAGUZI VIONGOZI RT


CHAMA cha Makocha wa Riadha Tanzania (CHAWARITA), kimelipongeza Baraza la Michezo la Taifa (BMT), chini ya Mwenyekiti wake, Dioniz Malinzi kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), uliofanyika mjini Morogoro Jumapili iliyopita na kupatika viongozi wapya chini ya Rais Anthony Mtaka.
Akizungumza mjini hapa, Katibu Mkuu wa CHAWARITA, Mwanariadha mahiri wa zamani, Nobert Kilimtali, alisema, wanampongeza Malinzi na Baraza kwa ujumla, kwa kuhakikisha mikoa yote Tanzania inafahamu kuna Riadha Tanzania na kuwaita Morogoro kushiriki katika uchaguzi huo.
Kilimtali alisema, pia wanawapongeza waliochaguliwa, ila watambue wamepewa madaraka na kuna kazi kubwa kuhakikisha wanaibua vipaji vya nyota wa zamani kama akina Filbert Bayi, Juma Ikangaa, Gidamis Shahanga, Zakaria Barrie, Gidamis Shahanga, Alfredo Shahanga, Mwinga Mwanjala, Rehema Killo, Zebedayo Bayo, John Yuda, Lwiza John na wengineo wengi.
“Pia uongozi mpya upokee changamoto ya kuhakikisha mchezo wa riadha unaanzia chini shuleni na unachezwa mikoa yote, tofauati na ilivyo hivi sasa,” alisema.
Katibu huyo, aliwapongeza wagombea waliothubutu ingawa kula zao hazikutosha, sambambna na viongozi waliokuwa madarakani na kukubali uchaguzi ufanyike na kuwataka wasisite kushirikiana na uongozi mpya.
Uongozi mpya wa RT uliongia madarakani Jumapili ya Mei 22 katika uchaguzi uliofanyika hoteli ya Hilux mjini Morogoro ni pamoja na Rais Anthony Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya (DC), ya Mvomero mkoani Morogoro, Makamu wa Rais Utawala, William Kallaghe, Makamu wa Rais Ufundi, Dk. Ahmed Ndee, Katibu Mkuu, Mujaya Suleiman Nyambui, Katibu Msaidizi, Ombeni Zavalla, Mweka Hazina, Is-Haq Suleiman, huku wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Mwinga Mwanjala, Meta Petro, Peter Mwita, Tullo Chambo, Rehema Killo, Lwiza John, Zakaria Barrie, Zakaria Gwanda, Robert Kalyahe na Christian Matembo.

Comments