LIUNDA KUSIMAMIA MECHI YA MCHUJO WA KOMBE LA DUNIA

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa Kamishna wa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia 2014 Kanda ya Afrika kati ya Lesotho na Sudan itakayochezwa jijini Maseru. Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itachezwa kati ya Juni 1 na 3 mwaka huu. Lesotho na Sudan ziko kundi D pamoja na Ghana na Zambia. Naye Hafidhi Ally ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa Kamishna wa mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Dynamos FC ya Zimbabwe na Esperance Sportive ya Tunisia. Mechi hiyo ya marudiano hatua ya 16 bora itachezwa Mei 13 mwaka huu kwenye Uwanja wa Rufaro jijini Harare. Esperance Sportive ilishinda mechi ya kwanza kwa mabao 6-0.

Comments