KUSOGEZWA PAMBANO LA WATANI:SIMBA KICHEKO,YANGA KILIO


WAKATI funga pazia la Ligi Kuu bara likisogezwa mbele kwa siku moja, watani Simba na Yanga wamepokea uamuzi huo kila moja kwa mtazamo wake.
Awali wakongwe hao walikuwa waumane kesho kwenye Uwanja wa Taifa, lakini kutoka na uamuzi wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), sasa wataumana Jumapili.
Klabu zote, licha ya kukubali kushuka dimbani Jumapili, zimeelezea kusikitishwa na uamuzi huo wa kusogezwa mbele, kwani umewaharibia programu zao na kuongeza gharama za uendeshaji, huku Yanga ikitaka ilipwe fidia.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’, alisema kuwa ingawa hawajazifurahia taarifa hizo, lakini wako tayari kushuka dimbani.
Alisema kusogezwa mbele kwa siku moja zaidi kwa mechi hiyo, kutawaongezea gharama kwa kuwa timu yao iko kambini visiwani Zanzibar, lakini hawana kinyongo.
Aliongeza kuwa kusogezwa mbele kwa mechi hiyo, kutawanyima pia muda wa kutosha wa kupumzika, wanapojiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahli Shendi ya Sudan, katika Kombe la Shirikisho (CAF).
Kwa upande wa Yanga, wameitaka TFF kugharimia gharama za siku moja iliyosogezwa.
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, aliiambia Tanzania Daima kuwa kutokana na jinsi walivyokuwa wamejipanga kwa gharama za kuiweka timu kambini, inawagharimu kuanza kutafuta fedha za ziada na kuitaka TFF kubeba jukumu hilo.
Nchunga alisema kikosi chao kiko kambini mjini Bagamoyo kwa ajili ya maandalizi na kuwa walikuwa wamejipanga na kujua kambi yao inamalizika kesho na kurejea jijini asubuhi tayari kwa pambano hilo.
Alifika mbali zaidi na kubainisha kuwa endapo TFF watashindwa kugharamia siku hiyo moja, basi wawalipe deni lao ambalo wanawadai, zaidi ya sh milioni 9, ili waweze kuhakikisha wanamudu kuwagharimia wachezaji wao kambini, ndani ya siku hiyo moja.
Akizungumzia madai hayo, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema wao sio ambao wamesogeza mechi hizo mbele, bali ni moja ya chombo cha shirikisho hilo, ambacho ni Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ambayo ndiyo iliyopendekeza mechi hizo kusogezwa.
“Mbona tulipokuwa tunasogeza mechi nyingine ama kuzirudisha nyuma, walikuwa hawalalamiki wala kusema kitu kama hicho na wanakuja kusema kwa sasa, sisi tumekisikiliza chombo chetu na ndiyo maana tukatangaza hivyo,” alisema Osiah. 

Comments