KUFUATIA HALI TETE YANGA SC, VIJANA YANGA KUKUTANA KESHO

UMOJA wa vijana wa Yanga kesho unatarajiwa kufanya mkutano maalum kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayoihusu klabu hiyo, mkutano ambao utafanyika makao makkuu ya klabu hiyo kuanzia saa nane mchana, imefahamika. Mwenyekiti wa umoja huo, Bakili Makele aliwaambia waandishi wa habari leo kwamba lengo la kufanya mkutano huo ambao aliuita ni wa amani tu ni katika kujadili baadhi ya mambo ikiwemo mwendeo iliyouonyesha timu yao kwenye ligi kuu soka Tanzania Bara, pamoja na masuala mengi ambayo yatailetea manufaa klabu hiyo katika siku za baadaye, kabla ya kuwasilisha kwa uongozi. “Tumetema ubingwa, pia kupata aibu ya kipigo cha mabao 5-0 toka Simba,sasa tunataka tufute aibu hii katika michuano ya Kagame kwa kutetea ubingwa wetu, hivyo tunahitaji tupate kikosi imara kinyume na hapo tunawezageuka kuwa sinema kwani sina imani kama kuna wachezaji watabaki au la,”alisema. Hata hivyo, Makele aliongeza kuwa iwapo uongozi utawazuia kufanya mkutano katika klabu hiyo wataamua la kufanya, huku akisema anaamini hilo halitatokea kwani wao ni wanachama halali na wana haki ya kufanya mkutano katika eneo hilo. Kauli hiyo ya Makele inafuatia hivi karibuni uongozi kuwazuia wazee wa baraza la klabu hiyo kufanya mkutano wao uliokuwa maalum kwa ajili ya kujadili masuala kama hayo, ambapo wazee hao wamekuwa katika msigano na uongonzi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Lloyd Nchunga baada ya kumtaka aachie ngazi kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio klabu hiyo..

Comments