KOCHA ZANZIBAR HEROES KUTAJA SILAHA ZA VIVA WORLD CUP

KOCHA mkuu wa timu ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Hemed Moroko, anataraji kutangaza kikosi chake kwa michuano ya Kombe la Dunia kwa mataifa yasiyo na uanachama wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa). Fainali za michuano hiyo, zimepangwa kufanyika Kurdistan, Iraq kuanzia Juni 4, mwaka huu. Ofisa Habari wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Muniri Zakaria, alisema kocha yuko hatua ya mwisho ya kukitangaza kikosi kitakachoshiriki michuano hiyo. “Yupo katika mchujo wa mwisho na muda mfupi anatarajia kukitangaza na kuanza kambi,” alisema Munir. Munir alisema mbali ya uteuzi huo kuzingatia uwezo wa wachezaji, pia suala la nidhamu ni kigezo muhimu kwa lengo la kuwa na timu bora. “Nidhamu itabeba sehemu kubwa ya uteuzi wetu, hatutowakaribisha wachezaji wenye nidhamu mbovu mchezoni na nje ya mchezo,” alieleza. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa ZFA, Alhaj Haji Ameir, msafara wa timu hiyo, utakuwa wa watu 26, ikiwemo kufanya ziara nchini Ujerumani. Jumla ya mataifa manane yanatarajiwa kushiriki michuano hiyo ya VIVA World Cup huku Zanzibar ikishiriki kwa mara ya kwanza. Zanzibar inayosaka uanachama wa Fifa kwa kipindi kirefu bila mafanikio, imejiunga katika umoja huo kwa lengo la kujitambulisha kimataifa nje ya sura ya Muungano. Tayari Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), limeshafanya jitihada kadhaa kuisaidia Zanzibar kupata uanachama huo.

Comments