KOCHA WA ZIMBABWE AIFAGILIA TWIGA STARS

WAKATI timu za Taifa za wanawake za Tanzania ‘Twiga Stars’ na Zimbabwe zinatarajiwa kukwaana keshokutwa, kocha mkuu wa timu ya Zimbabwe Rosemary Mugadza ameifagilia Twiga Stars na kusema kama itawezekana wangecheza mechi mbili za kirafiki. Timu hizo ambazo zitaumana katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kujinoa na michezo yao ya kimataifa ambapo Twiga inajiandaa kucheza na Ethiopia katika mechi ya kuwania mchujo wa kucheza fainali za Wanawake barani Afrika, huku Zimbabwe ikijiandaa na mchezo wake wa mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mugadza alisema kuwa wameamua kuja kujinoa kwa Twiga kutokana na kuwa moja ya timu zilizoonyesha kiwango kizuri katika michezo yake ya hivi karibuni hivyo watapata maandalizi ya kutosha. Alisema anaifahamu Twiga Stars baada ya kucheza nao mara mbili mwaka jana. Mara ya kwanza ilikuwa kwenye nusu fainali ya Kombe la COSAFA ambapo katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare, Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2, huku mara ya pili ilikuwa kwenye michezo ya All Africa Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo katika mechi yao iliyochezwa Septemba 11 timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. Mabao ya Twiga Stars yalifungwa na Asha Rashid na Mwanahamisi Shuruwa. “Pia Twiga Stars ilishacheza na Nigeria kwenye fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010 na kufungwa mabao 2-1, hivyo nadhani tutakuwa tumepata timu sahihi ya kujipima nayo. Kabla ya mechi ya kesho Zimbabwe ilicheza mechi ya kirafiki jijini Harare dhidi ya Zambia na kushinda mabao 2-1, huku Twiga Stars ikifanya ziara katika mikoa ya Dodoma na Mwanza na kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu inatarajiwa kuwasili jijini dare s Salaam leo. Ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura alisema jana kwamba maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yanakwenda vizuri ambapo viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi kimataifa Judith Gamba ni sh. 1,000 tu kwa sehemu zote isipokuwa VIP A ambayo ni sh. 10,000 na VIP B ambayo kiingilio chake ni sh. 5,000.

Comments