KIM POULSEN:MAMBO MAZURI HAYATAKI HARAKA

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema timu yake inaweza kufanya vizuri, lakini lazima wapewe muda.
Gazeti la Habari Leo, limeandika leo kwamba kutokana na hali hiyo amewaomba mashabiki nchini kuwa wavumilivu na kwamba ipo siku wataikubali na kuanza kuwashangilia wachezaji.
“Ni mwanzo mzuri wa safari yangu, kutoka sare nadhani ni mwanzo mzuri, sio matokeo mabaya kwangu na wala sio matokeo mabaya kwa Malawi, nahitaji kupewa muda zaidi,”alisem Kim baada ya mchezo wa kirafiki kati ya Stars na Malawi juzi uliomalizika kwa timu hizo kutofungana.
Alisema amefurahishwa na kiwango ambacho timu yake ilikionesha na kuomba kupewa
muda zaidi ili ifanye vizuri kwani kikosi chake bado ni kichanga na kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi hivyo hawezi kuibadilisha timu hiyo kipindi cha wiki moja tokea aanze kuifundisha timu hiyo.
Kocha huyo aliyekuwa akifundisha timu za taifa za vijana aliwataka wachezaji wa timu hiyo
kucheza vizuri muda wote ili kuwanyamazisha mashabiki wachache waliokuwa wakiizomea
kwenye mchezo huo.
“Ukiona mashabiki wanazomea ujue bado haujawafurahisha, nafikiri wakicheza vizuri hawatazomewa, naelewa hisia za mashabiki kuwa wanataka timu ishinde na ichezea vizuri lakini hilo lisipotokea ni wazi watazomea,”alisema Kim.
Taifa Stars itacheza na timu ya Taifa ya Ivory Coast Juni 2 huko Abdijani kujiandaa na mchezo wa awali wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.
Mbali na miamba hiyo ya soka ya Afrika Magharibi Stars iko kundi moja na Gambia na
Morocco. 

Comments