KESI YA LULU YAPIGWA KALENDA TENA, WAKILI ATAKA IPELEKWE MAHAKAMA YA WATOTO


Lulu alipofikishwa mahakamani mwezi uliopita chini ya ulinzi mkali. Leo ilikuwa kawaida tu.

UTATA kuhusu umri wa mtuhumiwa wa kesi ya mauaji, mwigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ leo umeanza kutoa matokeo, kwenye ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam, huku kesi yake ikipigwa tena kalenda hadi Mei 21, mwaka huu.
Lulu anayekabiliwa na kesi ya kumuua mwigizaji mwenzake, Steven Charles Kanumba, kwa sasa anasema ana miaka 17, lakini katika mahojiano kwenye kipindi cha TV cha Mikasi, kabla ya kifo cha The Great aliwahi kusema ana umri wa miaka 18.
Wakili wa mwigizaji huyo aliyekulia kwenye sanaa hiyo kuanzia akiwa kinda katika kundi la Kaole Sanaa la Magomeni pamoja na marehemu Kanumba, Kenned Fungamtama leo aliwasilisha ombi katika Mahakama hiyo, akiitaka iitupilie mbali kesi hiyo ili ikafunguliwe upya katika Mahakama ya Watoto, akidai Lulu ana umri chini ya miaka 18.
Lakini Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda alipinga akisema suala hilo, inabidi kwanza lifanyiwe uchunguzi na vyombo vya dola ili kugundua ukweli kuhusu umri wa Lulu(pichani kushoto).
Akizungumza mahakamani hapo, Wakili Kaganda alisema mbali na umri wa Lulu kuwa na utata, lakini hata jina lake halisi nalo ni tatizo, pia kwani wakati wengi wanamfahamu kama Elizabeth Michael, lakini cheti chake cha kuzaliwa kinasomeka Diana Elizabeth.
Katika ufafanuzi wake, Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando alisema analitupilia mbali ombi la upande wa utetezi, kwa sababu mtuhumiwa anakabiliwa na kesi ya mauji na imefunguliwa chini ya Kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Alisema kwa mujibu wa kesi hiyo, Mahakama yake haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo, zaidi ya Mahakama Kuu. Hakimu Mmbando ameiahirisha kesi hiyo hadi Mei 21, mwaka huu.
Tayari msisimko wa kesi hiyo unaonekana kuanza kupungua taratibu, kwani leo Lulu aliwasilishwa katika ulinzi wa kawaida na mahakamani hapo hakukuwa na idadi kubwa ya watu, kama ilivyokuwa alipofikishwa mahakamani mara ya pili, mwezi uliopita.