CHIPUKIZI 10 WAPITA MCHUJO ASPIRE


Wachezaji 10 wamepita katika mchakato wa kusaka vipaji kwa chipukizi wenye umri chini ya miaka 14 kupitia mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream ambao uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uliofanyika kuanzia Mei 21-26 mwaka huu. 
Watoto zaidi ya 1,500 walishiriki katika mchakato huo uliokuwa chini ya mng’amua vipaji (scout) Gisbert Xavier kutoka Hispania, na ulifanyika katika vituo vya Morogoro, Bagamoyo mkoani Pwani, na Kawe, Makongo, Magomeni, Tabata, Kitunda, Tandika, Ukonga na Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kwa Dar es Salaam. 
Kituo cha Morogoro amechaguliwa Karim Hussein wa Shule ya Sekondari Nanenane, kituo cha Magomeni ni Joseph Mushi wa Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere wakati kituo cha Tabata ni Martin Tangazi. 
Tandika ni Ismail Ngakonda (Shule ya Sekondari Uwanja wa Ndege), Kitunda ni Nicholas Lauteri (Shule ya Sekondari Ulongoni), Omari Mbwai (Shule ya Sekondari Msongola) na Hamad Omari (Shule ya Sekondari Ulongoni). 
Kituo cha Ukonga ni James Msuva (Shule ya Sekondari Makongo) wakati Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume ni Adolf Mtasigwa (Shule ya Sekondari Loyola) na Ally Hatibu (Shule ya Sekondari Kurasini). 
Mng’amuzi huyo wa vipaji anatarajia kufanya mchujo wa mwingine kabla ya chipukizi hao kwenda Nairobi, Kenya kwenye mchujo wa mwisho baada ya kambi ya ya siku nne kuanzia Juni 5-9 mwaka huu.


Comments