CANNAVARO, BABI KUIBEBA ZANZIBAR HEROES


KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya  Zanzibar, Zanzibar Heroes,  Hemed Suleiman 'Moroko', ametangaza kikosi cha nyota 18 kitachoshiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa nchi zisizo wanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), iitwayo  'Viva World Cup'.
Michuano hiyo itakayoanza Juni 4, nchini Kurdistan, Kaskazini mwa Iraq, itashindanisha mataifa tisa.
Ofisa Habari wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria, aliwataja wanasoka hao na timu wanazotoka kwenye mabano; ni Ismail Khamis (Mafunzo), Awadh Juma (Mtibwa Sugar), Khamis Mcha (Azam FC), Juma Othman Mmanga (Jamhuri), Mohammed Abdulrahim (Mafunzo), Abdulhalim Humoud na Abdughan Gulam  (Azam FC).
Wachezaji wengine ni Abbas Nassor (Miembeni United), Ali Badru (Al Canal, Misri), Amir Hamad (JKT Oljoro), Abdi Kassim  (Azam FC), Suleiman Kassim (African Lyon) na Nadir Haroub (Yanga).
Wengine ni Ali Mohammed (Super Falcon), Yussuf Makame (Mafunzo), Salum Shebe (Al Mudheiby, Oman), Sabri Ramadhan (Omani Club) na Gharib Mussa (African Lyon).
Ofisa huyo alisema, wachezaji wengine wanne wanaocheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara hawakuitwa kutokana na kuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa na mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Ivory Coast.
Nyota hao ni Nassor Masoud (Simba SC), Aggrey Morris, Waziri Salum na Mwadini Ali wanaocheza Azam FC.
Kikosi hicho tayari kimeanza mazoezi katika uwanja wa Mao Dzedong chini ya Moroko akisaidiwa na Hafidh Muhidin kujiandaa na michuano hiyo.
Wakati huo huo, timu ya Taifa ya Malawi inatarajiwa kuwasili  visiwani hapa Mei 28 kwa mchezo wa kukipima nguvu kikosi cha Zanzibar Heroes kabla ya kuanza safari ya kuelekea Kurdistan.
Zanzibar Heroes inatarajiwa kuondoka Juni 2  saa 4:20 asubuhi kwa ndege ya 'Precision Air' hadi Dar es Salaam ambako itapanda ndege ya Shirika la Air Qatar hadi mjini  Doha kabla ya kuunganisha safari ya Kurdistan.
                                                         

Comments