BOBAN APATA KIGUGUMIZI KUREJESHWA KWAKE STARS

MSHAMBULIAJI wa Simba Haruna Moshi 'Boban' ameingia kigugumizi kuhusiana na kurejeshwa kwake Stars. Mamapipiro blog ilimsaka kwa udi na uvumba Boban kuzungumzia kurejeshwa kwake kundi lakini aliishia kujiumauma kabla ya kuomba atafutwe baadaye kwani hajajipanga kwa maswali kutokana na ukweli kwamba ndo kwanza amerejea kutoka safari. Boban na timu yake ya Simba walirejea asubuhi ya leo kutoka nchini Sudan walipokwenda kurudiana na Al Ahli Shendi ya huko katika mchezo wa kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) kabla ya kutolewa kwa penalti 9-8. Jana kocha mpya wa Stars Kim Poulsen alimrejesha kundini Boban ambaye alitemwa kwenye kikosi hicho na kocha wa zamani wa Stars, Marcio Maximo, mwezi Machi mwaka 2009 kutokana na utovu wa nidhamu alioufanya na mwenzake Athuman Idd 'Chuji'.Chuji na Boban walidaiwa kuwakacha wenzao pindi waliporejea kutoka Ivory Coast walipokwenda kushiriki fainali za Afrika zinazoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) Hata hivyo mrithi wa Maximo, Jan Poulsen alimwita tena kundini Agosti mwaka jana na kumtaka Boban afanye kwanza mazoezi na wachezaji wa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 kilichokuwa kijiandaa na mchezo dhidi ya Shelisheli uliopigwa mjini Arusha mwaka jana, lakini alidai kuwa hana taarifa na wito huo. Jana kocha mpya wa Stars Kim Poulsen alitangaza kikosi cha Stars ambacho ndani yake kimesheheni wachezaji chipukizi zaidi, huku pia akiwatema wachezaji nguli wa timu hiyo wakiwemo Nahodha Shadrack Nsajigwa 'Fuso' na Nizar Khalfan. Aidha, mbali na Boban, Kim pia amewarejesha kundini mshambulaji wa Azam FC John Bocco 'Adeboyor' ambaye alitangaza kujitoa timu hiyo kwa madai ya kuzomewa na mashabiki p[indi anapokamata mpira, pia mshambuliaji wa Tanzania nayekipiga TP Mazembe ya Congo, Mbwana Samatta.

Comments