BAUSI AKATAA UTEZI ZFA

BEKI wa zamani wa kimataifa wa Zanzibar, Salum Bausi Nassor, amekataa uteuzi wa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha soka Zanzibar (ZFA), kwa lengo la kuendeleza mchezo huo. Hivi karibuni, Makamu wa Rais wa ZFA, Alhaj Haji Ameir, alimtangaza Bausi, aliyewahi kukipiga katika timu ya Zanzibar na Taifa Stars, kushika nafasi hiyo kutokana na uwezo wake. Akizungumzia kukataa kwake uteuzi huo, Baus amesema ni kutokana na kutokuwa na sifa ya nafasi hiyo ambayo mhusika hupaswa kuwa na walau kuanzia stashahada ya ukocha, sifa ambayo hana. Sababu nyingine ya kuikataa nafasi hiyo, ni dhamira yake ya kuitaka nafasi ya urais wa ZFA iliyoachwa wazi na Ali Ferej Tamim, aliyejiuzulu mwezi mmoja uliopita. “Nataka urais wa ZFA, sina haja ya ukurugenzi, tayari nimeshatangaza nia ya kuchukua fomu, najiandaa kwa hilo,” alisema. “Mkurugenzi wa Ufundi ni lazima uwe na diploma ya soka kama aliyonayo Sunday Kayuni wa TFF, mimi nina ‘advance certificate, sistahili.” Zaidi ya hilo, Bausi alikwenda mbali na kuhoji vipi ZFA ione sasa haja ya kumpa nafasi hiyo baada ya kutangaza azma yake ya kuwania urais, kwa nini hawakuwahi kufikiria hilo huko nyuma. Bausi alisisitiza nia yake ya kukiongoza chama hicho kwa ufanisi kama atapata ridhaa ya wapiga kura akishirikiana na wengine kutokana na Zanzibar kujaaliwa vijana wengi wenye vipaji vya soka.

Comments