BAADA YA UBINGWA BARA, SIMBA YAELEKEZA NGUVU ZOTE KOMBE LA SHIRIKISHO


SIMBA imeweka kando furaha ya ubingwa wake wa ligi kuu soka Tanzania bara na kuamua kuelekeza nguvu zake katika kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) ambapo keshokutwa wanatarijiwa kwenda Sudan kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya Al Ahli Shandy ya Sudan
Wekundu hao wa Msimbazi walikabidhiwa rasmi kombe la ubingwa jana baada ya kuwakandamiza mahasimu wao wa jadi nchini Yanga mabao 5-0 katika mchezo wa mwisho la ligi kuu soka Tanzania Bara uliopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam. 
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga ameiambia mamapipiro blog kwamba  wamefurahi kutwaa ubingwa huo lakini hawana budi kuelekeza nguvu zao katika kombe la Shirikisho ambapo kikosi cha Simba kinatarajiwa kuingia kambini leo jioni kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa marudiano dhidi ya Wasudan hao utakaopigwa mwishoni mwa wiki hii. 
Alisema kikosi chote cha timu hiyo kitaingia katika hoteli ya Saphire iliyopo katikati ya jiji kujiandaa na mchezo huo ambapo katika mechi ya kwanza iliyopigwa nchini wiki iliyopita Simba ilishinda mabao 3-0. 
Aliongeza kuwa taarifa zaidi juu ya safari hiyo zitatolewa baada ya kanmati ya utendaji ya Simba ambayo ilitarajiwa kukutana jana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya klabu hiyo. 
Aidha,Kamwaga amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kujituma kadiri walizoweza na hatimaye kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ambayo ilijaa upinzani wa hali ya juu na hasa ikizingatiwa kulikuwa na timu zaidi ya tatu zikiwania ubingwa huo. 
Pamoja na pongezi hizo, wachezaji wa timu hiyo wanatarajiwa kuizawadiwa ili kuwapa motisha kutokana na kazi nzuri waliyoifanya.

Comments