15 WAJITOSA MISS KIGAMBONI CITY 2012

Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya warembo 15 wamejitokeza kushiriki katika shindano la  kumsaka malkia wa kitongoji cha Kigamboni mwaka huu 'Miss Kigamboni City 2012' ambalo litafanyika Juni 15 kwenye ukumbi wa Navy Beach ulioko huko Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu  (pichani) alisema kuwa maandalizi ya shindano hilo yanaendelea vizuri na bado milango iko wazi kwa warembo wengine wanaotaka kuwania taji hilo ili kutoa nafasi ya kupata mwakilishi atakayefanya vyema kwenye ngazi ya kanda na taifa hapo baadaye.
"Bado hatujafunga milango, tunawakaribisha wasichana wenye sifa kujiunga ili tuweze kupata mshindi atakayepeperusha kitongoji cha Kigamboni vizuri," alisema mratibu huyo.
Alisema kuwa kampuni yake ya K & L iliyopata baraka za kuandaa shindano hilo imejipanga kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa bora na kuwapata washiriki watakaokwenda kutwaa taji la Kanda ya Temeke na hatimaye taji la taifa la Redd's Miss Tanzania baadaye mwaka huu.
Aliwataja warembo ambao wameshaanza mazoezi chini ya Hawa Ismail ambaye alikuwa Miss Temeke mwaka 2003 kuwa ni pamoja na Caroline Peter, Theopisther Wenso, Sophia Martime, Amina Aboubakar, Aisha Rajab, Rosemary Peter, Mariam Mbulilo, Julieth Phili, Doreen Kweka, Agness Goodluck, Khadija Kombo, Lina David, Aisha Mussa, Edda Silyvester, Fatina Francis na Rosemary Deogratius.
Alisema kwamba shindano hilo linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's, Dodoma Wine, Screen Masters, Clouds FM, Times FM na NSSF.
Taji la taifa la shindano hilo linashikiliwa na Salha Israel ambaye alitokea katika Kanda ya Ilala.

Comments

  1. YANGA BOMBA-UHURU BRANCHMay 30, 2012 at 9:05 PM

    nimeshtuka baada ya kusoma kichwa cha habari na kuona picha ya somoe,nikadhani na yeye ni mmoja wa hao 15 walioamua kujitosa miss kigamboni 2012 lol..!


    mdau wa bomba,boston,masachussetts

    ReplyDelete

Post a Comment