YANGA WAMPIGA MKWARA TIBAIGANA


WAKATI kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka Tanzania (TFF) ikitarajiwa kukutana kesho kwa ajili ya kujadili rufaa ya klabu ya Yanga kupokwa pointi, klabu ya Yanga imeitaka kamati hiyo kutoa maamuzi ya haki. 
Ofisa habari wa Yanga Louis Sendeu (pichani)amesema kwamba wameamua kutoa hadhari hiyo kutokana na utata uliopo katika suala hilo kwani wengi wameshindwa kuelewa sababu iliyopelekea Yanga kukata rufaa. 
Alisema wamekata rufaa kupinga kupokwa pointi taru na mabao matatu na kamati ya ligi kutokana na kumchezesha beki wao Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu alipopewa wakati Yanga ikicheza na Azam Fc ambapo kulitokea vurugu. 
“Maamuzi yalisema Cannavaro alipewa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu na si kumpiga mwamuzi...kikanuni anapaswa kukosa mechi mbili na ndivyo ilivyokuwa, lakini kama angepaswa kukosa mechi tatu tungeandikiwa barua,”Alisema. 
Sendeu aliongeza kuwa iwapo hawatarejeshewa pointi hizo walizopewa Coastal Union watakata rufaa kwenye kamati ya Rufaa ya TFF.
 Kamati hiyo nidhamu chini ya mwenyekiti wake Kamisha mstaafu wa polisi,Alfred Tibaigana itapitia na kutoa maamuzi ya rufaa hiyo ya Yanga ambayo kamati ya Ligi TFF iliipa Coastal Union ushindi kwa kuzingatia kanuni ya 25(f) ya Ligi Kuu ya Vodacom juu ya Udhibiti wa Wachezaji inayosema: “Ni lazima kwa klabu na wachezaji kutunza kumbukumbu za kadi. Klabu itakayomchezesha mchezaji mwenye kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu itapoteza mchezo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu (3) na mabao matatu (3), iwapo mchezaji atacheza akiwa haruhusiwi kucheza kwa ajili ya kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu timu yake itapoteza mchezo. Endapo klabu haina uhakika au inataka taarifa ya idadi ya kadi zake itaomba kwa maandishi toka TFF.” 
Kwa mujibu wa kamati ya Ligi, Cannavaro alioneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kupigana kwenye mechi kati ya Yanga na Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu ambapo kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi hiyo anastahili kukosa mechi tatu lakini alikosa  mechi mbili tu.

Comments